Skip to content

Serikali kuja na suluhisho tatizo la umeme

NA HAFSA GOLO

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kutumia zaidi ya shiling billioni 800 kwa ajili ya kutatua changamoto mbali mbali za umeme nchini ikiwemo kukatika mara kwa mara sambamba na upatikanaji wa umeme mdogo kwa baadhi ya maeneo. 

Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Nadir Abdul-latif, alieleza hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mafanikio yaliyopatikana katika siku 100 za uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kipindi cha pili cha uongozi wake, huko ukumbi wa Habari Maelezo Rahaleo.

Alisema serikali inaendelea kuchukua juhudi ili kuhakikisha inatatua changamoto ya ukosefu wa umeme nchini pamoja na kuahidi ifikapo mwaka 2028 Zanzibar itakuwa na umeme wa uhakika.

Waziri Nadir aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa, tayari serikali imeshaanza mchakato wa kutafuta miradi wezeshi ambayo itasaidia kuimarisha masuala ya upatikanaji wa umeme wa uhakika ikiwa ni pamoja na kusaini mikataba mbali mbali.

“Serikali imeshaingia katika mikataba mikubwa ya kubabadilisha laini zote kubwa za umeme Unguja na Pemba ambazo ni zaidi ya kilimita 1000”, alisema.

Aliitaja miongoni mwa hatua zitazochukuliwa kwa ajili ya utatuzi wa changamoto hiyo ni ununuzi wa transfoma kubwa nne zenye uzito wa tani 105 kwa kila moja, ununuzi wa meli ya muda ya umeme ambayo itakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme megawati 16 kwa kipindi cha miezi minane hadi mwaka mmoja. 

“Transfoma hizi zitakuja kutoa umeme wa uhakika, nzuri na bila ya kuyumba na tayari tushafunga minara kusini na Matemwe kaskazini mutaona mradi utakavyo kuwa mkubwa na kutoa huduma endelevu”, alisema Waziri Nadir.

Akizungumza changamoto ya kukatika ovyo umeme, alisema kuwa serikali imejipanga ndani ya kipindi Cha mwaka mmoja kuhakikisha changamoto hiyo inatatuka kwa kutumia mbinu mbadala ya matumizi ya umeme wa genereta.

Alifahamisha Nadir, kwamba hivi sasa serikali inafanya matengenezo makubwa ya majenereta yake ambapo kati ya 30 tayari 16 yameshafanyiwa matengenezo na majaribio ya awali huku mengine 14 yakiendelea na matengenezo ili yaweze kutoa huduma katika kipindi hichi cha mpito.

Sambamba na hilo, alisema serikali imeshafunga mradi wa sola na kampuni ya element kutoka nchini India ambapo mradi huo umegharimu dola milioni 159.

Mapema Nadir alisema, changamoto kubwa ya umeme sio kwa sababu ya umeme mdogo ni kutokana   na kuzidiwa kwa miradi mikubwa iliyojengwa katika kipindi cha serikali ya awamu ya nane inayoongozwa wa Dk. Mwinyi pamoja na uchakavu wa mindombinu. 

Alifahamisha kuwa umeme unaotoka Tanzania bara kupitia chini ya bahari ni na magawati 100, na mwengine wa ni 45 na magawati 20 kutoka Tanga kwenda Pemba ambapo kutokana na ujenzi wa miradi mikubwa na kuongezeka kwa idadi ya watu kwa sasa kiwango hicho hakiwezi kukidhi mahitaji ya sasa.

Hivyo alibainisha kuwa kwa sasa umeme uliopo ni magawati 135 lakini kilichozidi zaidi ya magawati 65 ambacho hakitoshi kwa mahitaji ya sasa na hasa kuongezeka kwa ujenzi wa miradi mikubwa.