Skip to content

Siku 100 za Uongozi wa Dk. Mwinyi

Serikali kuimarisha miundombinu, kuvutia wawekezaji, watalii

SERIKALI imesema inaendelea na ujenzi wa miundombinu muhimu hasa barabara, viwanja vya ndege na bandari ili kuchochea uchumi wa Zanzibar na kufungua maendeleo ya kijamii.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed, aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Unguja wakati akizungumza na Vyombo vya habari juu ya utekelezaji wa mafaniko ya siku 100 za Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kupitia wizara hiyo.

Alisema mikakati ya serikali ni kuhakikisha Zanzibar inakuwa na miundombinu bora na imara inayolingana na nchi nyengine duniani hasa katika usafiri wa anga, barabara na bandari.

Aidha Dk. Khalid alieleza kuwa ujenzi huo umedhamiria  kuleta mageuzi ya kiuchumi sambamba na kufungua fursa mpya za utalii hasa kwenye maeneo ya uwekezaji ikizingatiwa kuwa ni eneo muhimu linaloongeza pato la taifa.

Akifafanua kuhusiana na usafiri wa anga katika siku 100 za uongozi wa Dk. Mwinyi, Waziri Khalid alisema katika uwanja wa Abeid Amani Karume serikali imedhamiria kujenga Karakana ya ndege ili kuimarisha huduma bora.

“Katika utekelezaji wa hilo tayari wawekezaji watatu wameshajitokeza kwa ajili ya kuwekeza suala hilo ambalo linazingatia maslahi bora yanayoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia”, alisema.

Alitaja miundombinu mengine itakayojengwa eneo hilo ni pamoja na mnara mpya wa kuongozea ndege na vituo viwili vya mafuta ya ndege.

Akizungumzia kuhusu miundombinu ya barabara Waziri huyo alisema Serikali tayari imeanza maandalizi  ya ujenzi wa barabara mpya zenye urefu wa km 333.3 katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Alitaja miongoni mwa barabara hizo ni pamoja na ya Chanja Mjawiri – Tundaua yenye urefu wa kilomita 12.

Aidha Dk. Khalid alisema katika siku 100 hizo pia serikali imeanza ujenzi wa  barabara ya njia nne  ya Tunguu – Makunduchi yenye urefu wa km 48 ambapo Kampuni ya Mecco itahusika na ujenzi huo utakaozingatia viwango bora na mahitaji muhimu ya barabarani.

“Pia tunajenga barabara ya njia nne ya Fumba- Kisauni yenye urefu wa km 12, Dunga Mitini – Kilombero hadi Kinyasini yenye urefu wa km 19”, alisema.

Sambamba na hizo, lakini Dk. Khalid alisema tayari Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Bumbwini –Mfenesini yenye urefu wa km saba na hadi sasa ujenzi umefika asilimia 40.

Akigusia kuhusu ujenzi wa Fly Over ya Amani katika siku 100 za Dk. Mwinyi alisema umefikia asilimia 35 ambapo mwezi Mei mwaka huu unatarajiwa kukamilika.

Sambamba na hilo alisema kuwa siku 100 za Dk. Mwinyi serikali imeshafunga CCTV Kamera katika barabara ya Nyerere na Dole kwa ajili ya kulinda usalama wa abiria.

Akizungumzia kwa upande wa Pemba siku 100 za Dk. Mwinyi alisema upo utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Chake –Wesha, Mkoani –ChakeChake ambapo alisema zoezi na taratibu za ujenzi umeshaanza rasmini.

Kuhusiana na ujenzi wa bandari tayari baadhi yake zimeanza kujengwa ikiwa ni pamoja na bandari jumuishi ya Mangapwani na kutoa huduma za mafuta na gesi.