Skip to content

Mtandao mpya uingizaji dawa za kulevya Zanzibar wabainika

Mamlsks ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar kwa kushirikiana na Zanzibar Transnational Organized Crime Task Force (ZTOCTF) wamefanikiwa kuvunja mtandao wa usambazaji wa dawa za kulevya zilizokuwa zikiingizwa na kusambazwa nchini kwa mbinu mpya ya kuzichanganya katika bidhaa za kawaida za matumizi ya kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Kanali Burhan Zubeir Nassor, alisema walifanya operesheni maalum katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar na kubaini kuwepo kwa mtandao unaotumia bidhaa kama pipi, chocolate, korosho na shisha kuficha dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa Kamishna Nassor, dawa hizo zilikuwa zikiingizwa nchini na raia wa Romania anayefahamika kwa jina la Alexandru Rozescu, mkazi wa Mbweni, kupitia kampuni ijulikanayo kama Zebra Retail Investment.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akisambaza bidhaa hizo katika maeneo mbalimbali ndani ya Zanzibar na hata nje ya nchi, ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Zambia na Malawi na tayari amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Watuhumiwa wengine waliofikishwa mahakamani ni Nahid Bandar Imtiz (33) na Farhad Mustafa Gulam (33), wote raia wa Tanzania wenye asili ya India, waliokutwa na bidhaa hizo zinazodaiwa kuwa na viambata vya dawa za kulevya.

Kamishna Nassor alisema watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika katika kusaidia kuingiza, kusambaza au kunufaika na biashara hiyo haramu watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Katika operesheni hiyo, jumla ya kilo 7.448 za bidhaa zenye majina ya ELF Bar, Freshy Cocaine na LSD zilikamatwa ambapo bidhaa hizo zilikuwa zikionekana kama bidhaa halali za chakula na burudani, lakini uchunguzi umebaini kuwa zilikuwa na viambata vya dawa za kulevya.

Ukaguzi maalum ulifanyika katika maduka yaliyopo Paje, Jambiani, Mbweni na Shangani, ikiwemo Popeyes UK Treatz, Shop N’GO pamoja na ghala lililopo eneo la CTLA Mpendae ni baada ya kupatikana taarifa za kijasusi kuhusu kuhusika kwao katika biashara hiyo.

Aidha, vyombo vya usafiri vilivyokamatwa kuhusishwa na mtandao huo ni gari aina ya Toyota TownAce (Z695JD), Toyota Harrier (Z726KR), Toyota Alphard (Z721LT) pamoja na pikipiki sita aina ya TVS.

Kamishna Nassor alionya kuwa endapo dawa hizo zisingedhibitiwa, zingeweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kuongezeka kwa waraibu wapya hususan watoto chini ya miaka 18 na vijana, kuongezeka kwa matatizo ya afya ya akili, vifo vya ghafla, kupoteza uwezo wa kunusa pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu nchini.

Alitoa wito kwa wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kuwa makini na bidhaa wanazonunua au kuwanunulia watoto na vijana, hasa bidhaa mpya au zenye vifungashio visivyozoeleweka, ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya athari za dawa za kulevya.