Meli ya MV. Mapinduzi II inatarajiwa kuanza safari zake za kawaida za kusafirisha abiria na mizigo mnamo mwezi Machi mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Kisauni, Dk. Khalid Salum Mohammed, Waziri wa ujenzi na Uchukuzi, alisema meli hiyo itafanya safari zake kati ya Unguja- Pemba na Tanga kama ilivyokuwa awali.
“Kwa muda wa zaidi ya miaka minne meli ya MV Mapinduzi II ilikatisha shughuli za kusafirisha abiria na mizigo kutokana na chombo hicho cha usafiri baharini kuharibika, tuliipeleka chelezoni Mombasa na isharejea hivyo itaendelea na shughuli zake muda wowote kutoka sasa, lakini mapema mwezi ujao ni tegemeo letu”, alisema.
Waziri huyo alisema matengenezo yaliyofanywa yameirejesha meli hiyo kwenye ubora wake kama iliyokuwa awali, ambapo serikali imetumia dola milioni 2.8 hatua ambayo alibainisha kuwa itapunguza changamoto ya usafiri.
Alisema kilichomuhimu zaidi hadi serikali kuchukua uamuzi wa kuitengeneza meli hiyo, ni kuona inawaondolea wananchi wa Zanzibar changamoto ya usafiri wa baharini.
Dk. Khalid alisema hatua ya kuanza safari kwa meli hiyo kunatokana na kazi nzuri iliyofanywa na wataalamu kutoka kampuni ya Khoje kutoka nchini Korea Kusini, ambapo aliipongeza kampuni hiyo kwa kutekeleza vyema jukumu hilo.
“Serikali ilichukua uamuzi wa kuitengeneza meli yake ya MV Mapinduzi II tumetumia fedha nyingi, ili kuhakikisha inarudi katika ubora wake kwa ajili ya kuwapunguzia changamoto ya usafiri hasa wananchi wa Unguja na Pemba”, alisema waziri huyo.
Alisema meli hiyo itakapoanza kutoa huduma rasmi itafunga gati katika bandari mpya ya Mpigaduri, ambapo tayari imeshajengwa gati ndogo ambayo itawezesha meli hiyo kufanya maegesho.
Akizungumzia chanzo cha kuharibika kwa meli hiyo na kushindwa kufanyakazi kwa miaka kadhaa, alisema wataalam wa kampuni ya Khoje walipoifanyia uchunguzi kabla matengenezo walibaini hitilafu kwenye mfumo wa kupoozea mashine (cooling system).
“Hii ni meli ya kisasa ina mifumo ya kielektroniki, ilipotokezea hilitafu kwenye mifumo ya kupoozea mashine kulikuwa na mlio maalum ‘alarm’, lakini manahodha wetu hawakubaini maana ya mlio huo, mwishowe meli ikaharibika na kushindwa kutoa huduma”, alisema.
Katika kuhakikisha changamoto hiyo haijirejei, Dk. Khalid alisema serikali imeingia mkataba na wataalam wa kampuni ya Khoje kuendelea kuwepo kwa muda wa miaka miwili wakati meli hiyo ikiendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Alisema lengo la kuwabakisha wataalam hao ni kuhakikisha wanawapatia utaalam manahodha na wahandisi wazalendo katika kukabiliana na changamoto ndogo ndogo za kiufundi.
