Na Saida Issa, Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Mzee Kasore, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kuwapatia vijana ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Ambapo ameeleza kuwa dhamira hiyo inalenga kujenga taifa lenye nguvu kazi yenye ujuzi wa vitendo unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jitihada za kuendeleza ufundi stadi na fursa zilizopo kwa vijana, CPA Kasore alieleza kuwa msimamo wa VETA ni kuhakikisha mafunzo hayo yanapatikana kwa wananchi wote bila kujali kiwango cha elimu, jinsia, hali ya kimwili au eneo analotoka mwananchi.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikipanga na kutekeleza afua mbalimbali zinazolenga kufikia maono ya maendeleo ya taifa yanayoendana na Dira ya Maendeleo 2050, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, Mpango Mkakati wa Kuendeleza Ujuzi Nchini pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025.

“Mpango wa VETA unalenga pia kuwezesha watu wenye mahitaji maalum, wakiwemo wenye ulemavu, kupata fursa zaidi za kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ili wapate ujuzi, kuajiriwa au kujiajiri,
mwaka huu VETA imefadhili wanafunzi 195 wenye ulemavu waliodahiliwa katika vyuo vya mamlaka hiyo kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu, ambapo ada zao zitalipwa kwa miaka yote ya masomo kuanzia ngazi ya kwanza hadi ya pili,”alisema.
Aidha alitoa wito kwa wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kuwaleta katika vyuo vya VETA ili waweze kupata stadi zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi na kimaisha.
“Uwekezaji katika ujuzi ni njia bora ya kuwajengea vijana na makundi maalum uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa,
mwamko wa vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi unaendelea kuongezeka, akieleza kuwa mwaka huu jumla ya waombaji 134 waliodahiliwa katika mafunzo ya muda mrefu ni wahitimu wa Astashahada, Shahada na Shahada za Uzamili,”alisema.
Kadhalika aliwataka wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu kutumia fursa ya mafunzo ya ufundi stadi kuongeza ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira.
“Dunia ya leo haihitaji vyeti pekee, inahitaji uwezo wa kufanya kazi,Ujuzi ni mtaji, ujuzi ni ajira, ujuzi ni kujitegemea, na ujuzi ni heshima,”alisema.

