Skip to content

Wafanyabiashara wa mbao, wagonga vyuma kuhamishiwa Sebleni

  • Zanzibar

NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya wilaya ya Mjini kwa kushirikiana na Manispaa ya Mjini inatarajia kutekeleza mpango maalum wa upangaji wa mji kwa kuwahamisha wafanyabiashara wanaojishughulisha na uchongaji, gereji, uuzaji wa mbao katika eneo la Sebleni.

Katibu Tawala wa wilaya ya Mjini, Dk. Said Haji Mrisho, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kulitembelea eneo  linalotarajiwa kupelekwa wafanyabiashara hao.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa serikali wa kuhakikisha mji wa Zanzibar unakuwa na mpangilio mzuri, mazingira safi na shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika maeneo yaliyo rasmi na yanayokidhi vigezo vya kisheria na kimazingira.

Alisema eneo la Sebleni limesafishwa na linaendelea kuimarishwa na kuwekewa miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na mipaka ya maeneo ya biashara, njia za kupitisha watu na magari pamoja na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wananchi, kupitia ushirikiano kati ya Baraza la Manispaa ya Mjini na kampuni ya ujenzi ya CRJE ya China.

Dk. Mrisho alibainisha kuwa wilaya ya Mjini ina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 16 pekee, hali inayohitaji matumizi ya ardhi kufanyika kwa mipango madhubuti na yenye kuzingatia maslahi ya sasa na ya baadae ya wananchi.

“Shughuli nyingi za kiuchumi, kijamii na kiutawala zote zipo ndani ya mji, kwa ukubwa huu mdogo wa eneo, hatuna budi kupanga matumizi ya ardhi kwa umakini mkubwa”, alisema.

Aliongeza kuwa serikali inalenga kuhakikisha wafanyabiashara wanakuwa katika maeneo yanayostahiki, ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato, kuimarisha usalama, kulinda afya ya jamii na kupunguza msongamano usio wa lazima katika barabara na maeneo ya umma.

Hata hivyo alisema Baraza la Manispaa ya Mjini litaendesha zoezi la uhakiki kwa wafanyabiashara wote wa mbao kabla ya kuwapangia maeneo rasmi ndani ya Sebleni, ili kuwepo mpangilio mzuri utakaowezesha kila mfanyabiashara kuendelea na kazi zake bila usumbufu.

Alisema baada ya kukamilika zoezi hilo kwa wafanyabiashara wa mbao, serikali itaendelea na awamu nyengine kuwahamishia na kuwapangia maeneo wafanyabiashara wa gereji za vyombo vya maringi mawili, matatu na manne, ambao kwa sasa wanapangiwa eneo maalum katika eneo la Karakana ili kukusanya huduma zote za gereji sehemu moja.

Dk. Mrisho alibainisha kuwa mkakati huo pia utawahusisha wagonga vyuma wa Mayugwani (Gulioni), ambapo nao watatafutiwa maeneo yenye mazingira bora, salama na rafiki kwa shughuli zao, ili kuondoa usumbufu kwa wananchi, kuruhusu barabara zipitike kwa urahisi na kuifanya mji uwe katika mpangilio unaoendana na hadhi ya Zanzibar.

Alisisitiza kuwa zoezi la upangaji wa wafanyabiashara ni endelevu na halitalenga kuwabana au kuwaondolea wananchi riziki zao, bali ni kuwasaidia kufanya biashara zao katika mazingira bora, rasmi na yenye fursa zaidi za kukuza uchumi.

“Serikali haitaki kuwakwamisha wafanyabiashara,tunachofanya ni kuwawezesha wafanye kazi zao katika mazingira bora zaidi, yenye usalama, usafi na yanayotambulika kisheria,” alisema.

Hivyo, aliwataka wafanyabiashara na wananchi  kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali wakati wa utekelezaji wa mpango huo, akieleza kuwa mabadiliko hayo ni muhimu ili kuendana na kasi ya uchumi, usafi wa mazingira na upangaji wa miji ya kisasa.

Alisema mpango huo unaendana na maono ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya kujenga miji iliyo safi, iliyopangika na inayoendana na maendeleo ya dunia bila kupoteza silka, utamaduni na asili ya Mzanzibari.

Nao baadhi ya wafanyabiashara wa mbao wanaofanya  shughuli zao Kijangwani na Amani Fresh walisema wapo tayari kushirikiana na serikali ilimradi wapatiwe maeneo yenye uhakika, huduma muhimu na mpangilio mzuri utakaowawezesha kuendelea kujipatia kipato bila usumbufu.

“Sisi tupo tayari kuondoka ikiwa serikali itatuweka katika mazingira mazuri yenye mahitaji yote muhimu kwani tunajua lengo la serikali yetu ni kuweka mji katika mazingira ya kupendeza,” alisema Juma Salim mfanyabiashara wa Amani.