NA MWANDISHI WETU, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ameihakikishia Japani kwamba itaendeleza uhusiano na mashirikiano yaliyodumu kwa muda mrefu na nchi ya Japani.
Makamu huyo ameyaeleza hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yoichi Mikami hafla iliyofanyika ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Alisema uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na Japan utaendelea kukuza mashirikiano katika pande zote mbili katika kuimarisha sekta za kilimo, biashara, maji safi na salama, maendeleo ya viwanda, utalii na miundombinu mbali mbali.
Hemed alisema serikali inaikaribisha serikali ya Japan katika kutumia fursa zilizopo katika uwekezaji hasa katika sekta ya utalii, uchumi wa buluu, kilimo na matumizi ya teknolojia kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.
Kwa upande wake, balozi wa Japan nchini Tanzania, Yoichi Mikami aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupiga hatua za maendekeo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kwamba ameahidi kuendeleza ushirikiano ulipo kati ya Tanzania na Japan.
