NA SELEMAN TAMBULEGENI
MKURUGENZI Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Nassor Shaaban Ameir, amesema Serikali ya Awamu ya Nane, imeweka utaratibu mzuri wa usafiri wa umma unaolenga kupunguza adha inayowakabili wananchi wanaotumia huduma hiyo kila siku.
Nassor aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili kwa mabasi mengine matano yanayotumia nishati ya umeme katika Kituo cha Daladala cha Kijangwani, mjini Unguja.
Alisema wiki tatu zilizopita ZSSF iliingiza mabasi 10 ya umeme kwa ajili ya usafiri wa umma na hivi karibuni idadi hiyo imeongezeka kwa kuwasili mabasi mengine matano ambayo tayari yapo katika kituo cha Kijangwani.
Alifahamisha kuwa jukumu la kupanga mgawanyo wa mabasi hayo kwa mujibu wa idadi ya abiria wanaotumia kila njia ni la Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, huku ZSSF ikipokea maelekezo kutoka mamlaka hiyo kulingana na mahitaji na wakati husika.
“Mpaka sasa tuna jumla ya mabasi 15 hapa Zanzibar na mengine yataendelea kuwasili kadiri miundombinu ya barabara inavyokamilika, serikali ya Rais Dk. Hussein Mwinyi inatekeleza kwa haki jukumu la kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kasi kubwa”, alisema Nassor.
Aliwatoa hofu madereva wa daladala ambao wana wasiwasi wa kupoteza ajira zao kutokana na ujio wa mabasi hayo, akieleza kuwa makubaliano kati ya ZSSF na waendeshaji wa mradi huo ni kuajiri madereva wazawa.
Alisema hadi sasa madereva 30 waliokuwa wakifanya kazi kwenye daladala tayari wameajiriwa kuendesha mabasi hayo ya umeme.
Aliongeza kuwa kabla ya kuwaajiri, ZSSF ilishirikiana na viongozi wa madereva pamoja na mamlaka zinazosimamia usafiri barabarani na kuthibitishiwa kuwa madereva hao wanakidhi vigezo vinavyohitajika.
Alisema utaratibu huo utaendelea kadiri mabasi yanavyozidi kuwasili Zanzibar.
Nassor alisema mpango wa jumla ni kuleta mabasi 100 ya umeme, huku yale yaliyopo kwa sasa yakikamilishiwa baadhi ya vifaa muhimu vikiwemo alama za kumtahadharisha dereva, taa za ndani, kamera za ulinzi, maandishi yanayoonesha upatikanaji wa viti, pamoja na maeneo maalumu kwa watu wenye mahitaji maalumu.
Alieleza kuwa mabasi 10 ya awali tayari yamekamilishiwa vifaa hivyo na wiki hii yatapelekwa kwa mkaguzi ili kupata kibali cha kuanza kutoa huduma, huku mabasi mapya yakifuata utaratibu huo huo.
Alisema ZSSF kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani tayari imekamilisha zoezi la kupima masafa ya vituo vya mabasi hayo kwa njia ya Uwanja wa Ndege na Buyu, kwa ushirikiano na Wizara ya Mawasiliano.
Kuhusu uendeshaji wa mradi huo, Ameir alisema ZSSF ni mwekezaji mkuu lakini kutokana na masuala ya uzoefu, waliona ni muhimu kushirikiana na kampuni yenye uzoefu wa kutosha kuendesha mradi huo, huku ZSSF ikibaki kuwa msimamizi mkuu wa uwekezaji huo.
Kwa upande wake, Kassim Suleiman, mkazi wa Fuoni mjini Unguja na mtumiaji wa usafiri wa umma, aliisifu serikali kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya usafiri, akisema ujio wa mabasi ya umeme ni hatua kubwa kuelekea usafiri wa kisasa.
Alisema usafiri huo utapunguza msongamano wa abiria katika vituo vya daladala na kuondoa usumbufu kwa wananchi, hususan akina mama wanaonyonyesha ambao mara nyingi wamekuwa wakichelewa kurejea majumbani mwao hadi usiku kutokana na changamoto ya usafiri wa umma, hali iliyosababisha wengine kuwakuta watoto wao tayari wamelala.
Alisema changamoto hiyo sasa inaelekea kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na kila mwananchi atanufaika kutokana na mradi huo.
