Skip to content

Saif al-Islam Gaddafi auawa

ZINTAN, LIBYA

SAIF al-Islam Gaddafi, mtoto wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, ameuawa kupitia kile ofisi yake ilichosema ni kitendo cha kihalifu na cha woga katika mji wa magharibi mwa nchi hiyo, Zintan.

Kifo cha mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 53, ambaye hapo awali alionekana kuwa mrithi wa baba yake, kilithibitishwa na mkuu wa timu yake ya kisiasa.

Kwa mujibu wa wakili wake, Khaled al-Zaidi, Saif aliuawa na watu wanne waliokuwa wameficha sura zao walioivamia ofisi yake siku ya mnamo Februari 3 mwaka huu.

Hata hivyo, dada yake alitoa taarifa zinazokinzana na hizo akiambia televisheni ya Libya kwamba alifariki karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.

Kituo cha televisheni cha al-Arabiya, kimeripoti kwamba Saif, aliyekuwa na umri wa miaka 53, aliuawa akiwa kwenye bustani ya nyumba yake huko Zintan, kikimnukuu mtu wa karibu na familia ya Gaddafi.

Kulikuwa na uvumi kwamba wanamgambo walio karibu na serikali yenye makao yake mjini Tripoli inayoongozwa na waziri mkuu Abdul Hamid Dbeibeh wamehusika na mauaji hayo, ingawa wenyewe wamekanusha.

Saif al-Islam Gaddafi kwa muda mrefu alionekana kama mtu mwenye ushawishi mkubwa na anayeogopwa zaidi nchini baada ya baba yake, ambaye alitawala Libya kuanzia 1969 hadi alipoondolewa madarakani na kuuawa wakati wa uasi mwaka 2011.

Hadi kifo chake, mtoto huyo wa Gaddafi alikuwa akitakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kujibu mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu wakati wa machafuko ya Libya.