Skip to content

Serikali yashauriwa kutunga sheria maalum ya ugatuaji

  • Bara

SERIKALI YASHAURIWA KUTUNGA SHERIA MAALUM YA UGATUAJI

Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdalah Chikota, ameitaka Serikali kuja na sheria maalum ya ugatuaji ili kuweka wazi majukumu ya Serikali Kuu na yale ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, akisema kuwa kwa sasa ugatuaji nchini unatekelezwa zaidi kwa matamko ya kisera kuliko misingi ya kisheria.

Akichangia Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano bungeni, Chikota amesema sheria hiyo itasaidia kubainisha vyanzo vya mapato na fedha kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, jambo litakalowezesha halmashauri kutekeleza majukumu yake kwa uhakika na uwazi zaidi.

Amesema kukosekana kwa sheria ya ugatuaji kumesababisha mkanganyiko wa majukumu kati ya viongozi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, hali inayochangia utolewaji wa matamko yanayokinzana na kuathiri utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi.

Aidha, Mbunge huyo ametaka kufanyika kwa tathmini ya kina juu ya uendeshaji wa mamlaka za serikali za mitaa, ikiwemo kuangalia kama bado kuna haja ya mabaraza ya madiwani kuendelea kuwa mamlaka ya nidhamu kwa halmashauri ili kuepuka masuala ya udanganyifu na changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa uwajibishwaji ndani ya halmashauri.