Skip to content

Mwenyekiti ZEC aidhinisha kuteketezwa nyaraka za uchaguzi

  • Zanzibar

NA KHAMISUU ABDALLAH

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), imeidhinisha rasmi zoezi la kuteketeza nyaraka zote zilizotumika katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025, baada ya kutimia muda wa siku 90 tangu kumalizika kwa uchaguzi huo.

Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha Tume kilichofanyika katika ofisi za Tume hiyo zilizopo Maisara mjini Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George Kazi, alisema zoezi hilo linafanyika kwa kuzingatia kifungu cha 98(3) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018.

Alisema kifungu hicho kinaitaka ZEC kuharibu nyaraka zote zinazohusiana na uchaguzi mkuu baada ya kupita siku 90 tangu kukamilika kwa zoezi la uchaguzi mkuu.

Aidha alisema kabla ya kuidhinisha utekelezaji wa zoezi hilo, ilijiridhisha kuwa hakuna amri yoyote ya mahakama inayozuia utekelezaji wa hatua hiyo, hali iliyoiwezesha kutekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa sheria baada ya kukamilika kwa muda uliopangwa.

Hivyo aliwataka wadau wote wa Uchaguzi kushirikiana ipasavyo katika utekelezaji wa zoezi hilo ili kuhakikisha linafanyika kwa mafanikio, uwazi na kuzingatia kikamilifu misingi ya kisheria na taratibu zilizowekwa.