Skip to content

Serikali yaendelea kuimarisha kingo za mito rau na ghona kudhibiti mafuriko

  • Bara

Na Saida Issa,Dodoma

MBUNGE wa Vunjo,Enock Zadock Koola, ameiuliza Serikali ni lini itaendelea kuimarisha kingo za Mto Rau na Mto Ghona ili kudhibiti mafuriko, kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni.

Akijibu swali hilo bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt.Jafar Seif amesema kuwa Mto Rau na Mto Ghona ni mito midogo iliyopo katika Bonde la Pangani, ndani ya Kidakio cha Mto Ruvu, ambacho huanzia katika miteremko ya Mlima Kilimanjaro na kusafirisha maji hadi Mto Ruvu, unaoyapeleka maji hayo katika Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za usimamizi wa mazingira kwa kulinda na kuzuia uharibifu wa kingo za mito hiyo,Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilitoa shilingi milioni 252 kwa ajili ya kazi ya kuondoa mchanga katika mito hiyo kwa urefu wa jumla wa mita 12,642.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kazi hizo zilitekelezwa katika Kata za Msaranga, Mjimpya, Kiboroloni na Mfumuni, hatua iliyolenga kupunguza athari za mafuriko katika maeneo hayo.

Aidha, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bonde la Mto Pangani itaendelea kuimarisha kingo za Mto Rau na Mto Ghona kwa kupanda miti, kutoa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira, pamoja na kuweka zuio kwa wananchi wanaolima na kujenga karibu na mito hiyo, ili kuepuka madhara yatokanayo na mafuriko wakati wa msimu wa mvua.

Serikali imesisitiza kuwa juhudi hizi ni sehemu ya mkakati endelevu wa kulinda mazingira na kuhakikisha usalama wa wananchi wanaoishi maeneo yanayopitiwa na mito hiyo.