Skip to content

HESLB Yazindua Mfumo wa AI Kuimarisha Huduma za Mikopo ya Elimu ya Juu

  • Bara

Na Saida Issa,Dodoma

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua rasmi mfumo wa kidijitali unaotumia Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) kwa ajili ya kuhudumia wateja wake, maarufu kama Bwana Bumu na Bibi Bumu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na ubora wa huduma kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika leo Jumatano, Januari 28, 2026, jijini Dodoma. Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) wa HESLB, Bahati Singa, amesema mfumo huo umeunganishwa moja kwa moja na mifumo ya mikopo ya bodi na una uwezo wa kuchakata taarifa kwa haraka na kwa usahihi kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya akili bandia.

Singa ameeleza kuwa kabla ya maboresho hayo, bodi ilikuwa ikitumia mbinu za kawaida kuwafikia wanufaika, hali iliyowezesha kuhudumia idadi ndogo ya watu kati ya 5,000 hadi 6,000 pekee. Hata hivyo, kutokana na uboreshaji wa mifumo, HESLB kwa sasa ina uwezo wa kuwafikia zaidi ya walengwa 10,000, huku ikitarajiwa idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia kati ya watu 100,000 na 200,000 kupitia mfumo wa Bwana Bumu na Bibi Bumu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bili Kiwia, amesema uzinduzi wa mfumo huo ni sehemu ya mageuzi makubwa ya utoaji huduma kwa wateja, akibainisha kuwa mfumo huo utakuwa ukitoa huduma kwa saa 24 kila siku, siku saba kwa wiki, mwaka mzima. Alisema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza malalamiko kutoka kwa wanufaika wa mikopo.

“Tunajivunia kuanzisha mfumo huu ndani ya nchi kwa kutumia wataalamu wetu wenyewe, badala ya kutegemea teknolojia kutoka nje pekee,” amesema Kiwia.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema mfumo huo utaimarisha uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, sambamba na kuongeza uelewa wa wadau kuhusu shughuli za HESLB.

Profesa Mushi ameongeza kuwa matumizi ya mfumo huo yanatarajiwa kupunguza gharama za utoaji wa huduma za mikopo kwa takribani asilimia 60, hatua itakayoongeza ufanisi na tija katika utendaji wa bodi. Aidha, amewahimiza wazazi na walezi kujifunza kuutumia mfumo huo ili kupata taarifa sahihi kwa wakati, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa taarifa na ushirikishwaji wa makundi yote, ikiwemo watu wenye mahitaji maalum.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, Jackline Humbaro, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema mfumo huo mpya utapunguza usumbufu kwa wanafunzi, hususan safari za mara kwa mara kufuata huduma za mikopo.

Uzinduzi wa Bwana Bumu na Bibi Bumu umetajwa kuwa hatua ya kihistoria katika mageuzi ya utoaji wa huduma kwa wateja ndani ya sekta ya elimu nchini.