Skip to content

Mavunde awaonya maofisa madini

  • Bara

NA SAIDA ISSA, DODOMA

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameonya kuwa serikali itachukua hatua kali dhidi ya maofisa watakaobainika kusababisha au kuchochea migogoro katika shughuli za uchimbaji, huku akisisitiza uzingatiaji wa Sheria na Kanuni za Madini.

Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi kikao cha Menejimenti cha Tume ya Madini kilichowakutanisha Wakurugenzi, Mameneja na Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa, kilicholenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka, pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika Sekta ya Madini.

Alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya maofisa katika Ofisi za Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa wanaochangia migogoro ya mara kwa mara kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini kwa kutoa leseni kwa waombaji wasiostahili, hali inayosababisha malalamiko na migongano baina ya wachimbaji.

“Nikiona kwenye ofisi yako kuna migogoro ya wachimbaji wa madini na kujiridhisha bila shaka kuwa ofisi inahusika, sitasita kuchukua hatua kali ikiwemo kukuondoa kwenye nafasi uliyokuwa nayo”, alisema Mavunde.

Aliagiza Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki, uwazi na weledi katika utoaji wa huduma, sambamba na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kuomba leseni za madini kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya uwekezaji.

Kadhalika Waziri Mavunde aliwataka Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwasilisha ndani ya siku saba orodha ya leseni kubwa za utafiti wa madini zisizofanyiwa kazi, ili hatua za kisheria zichukuliwe ikiwemo kuandikiwa hati za makosa na kufutiwa leseni hizo.

Aidha, alimtaka Mkurugenzi wa Leseni kuwasilisha orodha ya kampuni zenye leseni kubwa za utafiti kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wake.

Pia alimtaka Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha kuwa kabla ya Juni 30, 2026, mfumo wa e-leseni unaowezesha wateja kupata huduma bila kufika ofisini unaanza kufanya kazi kikamilifu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma.

Mavunde aliwataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanazifanyia kazi leseni walizopewa, akionya kuwa leseni zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitachukuliwa hatua ikiwemo kufutwa na kupewa wawekezaji wengine wenye dhamira ya dhati.

Aidha aliwaagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwasilisha kabla ya Februari 28, 2026, taarifa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanawake na vijana kupitia Mradi wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT).

Katika kuimarisha utendaji kazi, Waziri Mavunde alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, hususan katika kushughulikia changamoto za sekta, huku akiwahimiza kusimamia maadili ya watumishi walio chini yao, akibainisha kuwa wao ndiyo taswira ya Wizara ya Madini kwa wananchi.

Kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Januari 22, 2026, Serikali tayari imekusanya shilingi bilioni 719, sawa na asilimia 59.9 ya lengo la shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026,Hii ni hatua nzuri na nina imani kubwa kuwa tutavuka lengo lililowekwa na Serikali kabla ya Juni 30, 2026,”alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, alimpongeza Waziri Mavunde kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Wizara na taasisi zake zitaendelea kushirikiana kwa karibu ili Sekta ya Madini izidi kuimarika.