BARAZA la 11 la Wawakilishi mkutano wa kwanza, unatarajiwa kuanza leo ambapo litakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa spika.
Katibu wa Baraza la Wawakilishi Raya Issa Mselem, aliyasema hayo jana wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika ukumbi wa Baraza Chukwani.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 73 (1), wajumbe wateule wa baraza watamchagua mjumbe mmoja miongoni mwao au mwenye sifa za kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa Spika.
Katibu huyo alisema shughuli hiyo pekee ambayo mjumbe Mwakilishi anaweza kuifanya bila ya kula kiapo cha uaminifu ambapo ni kifungu cha 70 cha katiba.
Alibainisha kuwa shughuli nyengine ni Katibu wa Baraza kumuapisha Spika mteule kuwa spika wa Baraza na kiapo cha uaminifu cha wajumbe ambapo Spika atawaapisha kiapo cha uaminifu wajumbe wote ambapo nayo inatokana na masharti ya katiba kifungu cha 70.
Raya, alisema baraza hilo pia litakwenda sambamba na uchaguzi wa naibu spika ambapo ni miongoni mwa shughuli za mkutano wa kwanza zilizoelekezwa na kifungu cha 74 (2) cha Katiba ya Zanzibar na kanunu ya 19 (1) ya kanuni za kudumu za Baraza la Wawakilishi toleo la 2024.
Alibainisha kwamba pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi atazindua baraza hilo na kutoa maelekezo yake.
Wakati huo huo, baadhi ya wanachama kutoka vyama vya siasa wamejitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya spika wa Baraza la Wawakilishi.
Wa kwanza aliyejitokeza ni aliyekuwa Spika wa Baraza la 10 Zubeir Ali Maulid kutoka CCM, alisema ana imani na chama chake na ndio maana hawajajitoleza watu wengine kugombea nafasi hiyo.
Alisema anaimani na wajumbe watamchagua katika nafasi kwa kuamini ana uzoefu kwani hicho ni kipindi cha tatu kushika nafasi hiyo kama atachaguliwa.
Naye Mgombea wa nafasi hiyo, Suleiman Ali Khamis ambae ni Katibu wa Vijana taifa chama cha ADC, alisema kwa mujibu wa kauli ya Rais kutoa kauli ya kuwataka vijana kuhamasika na kujitoa kugombea nafasi mbalimbali.
Alisema kwa mujibu wa vigezo alivyonavyo anastahiki kupata nafasi hiyo kwani vigezo vyote ametimiza ikiwemo elimu, umri wa kupigia kura na utayari wake kusimama kuongoza.
Majina mengine yaliyopokelewa katika baraza kugombea nafasi hiyo ni Naima Salum Hamad UDP na Chausiku Khatib Mohammed NLD.
