Skip to content

Kikao cha kwanza cha bunge kuanza Novemba 13

  • Bara

KATIBU wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraka Leonard, amesema kikao cha kwanza cha bunge la 13, kinatarajiwa kuanza Novemba 11 mwaka jijini Dodoma.

Katibu huyo ameyaeleza hayo jana kwenye taarifa aliyoitowa kwa vyombo vya habari, iliyolenga kuwaita wabunge wateule kufika jijini Dodoma kuhudhuria mkutano wa kwanza wa bunge la 13.

Katika taarifa hiyo, katibu huyo alisema kuwa katika mkutano huo wa kwanza kutafanyika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusomwa tangazo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuitisha bunge.

Leonard alisema shughuli nyengine ni wabunge wateule kumchagua Spika atakayeuongoza muhimuli huo wa dola na wabunge wote kula kiapo cha uaminifu.

Aidha alizitaja shughuli nyengine katika kikao hicho ni kuthibitisha uteuzi wa waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi wa naibu spika na ufunguzi rasmi wa bunge jipya utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika wito huo wa wabunge wateule kuitwa bungeni Dodoma, Katibu huyo amewasisitiza kuhakikisha wanazingatia kikamilifu kuvaa mavazi rasmi kwa ajili ya usajili na upigaji picha.

Katibu huyo aliwataka wateule hao wafike kwenye chombo hicho wakiwa na hati za kuchaguliwa ama kuteuliwa, kitambulisho cha taifa na nakala yake, kadi ya benki yenye namba ya akaunti ya bunge.

Nyaraka nyengine walizosisitizwa kuwa nazo ni cheti halisi cha ndoa kinachotambuliwa na serikali kwa wenye ndoa, sambamba na nakala ya cheti hicho.

Wateule hao pia wametakiwa kuwasilisha vyeti halisi vya kuzaliwa vya watoto wenye umri wa miaka 21 kwa wenye watoto wasiozidi wanne na nakala za vyeti hivyo.

Leonard pia aliwataka wateule hao kuwasilisha vyeti vya elimu na taaluma vyenye ithibati ya taasisi husika na nakala zake pamoja na wasifu wa mbunge mteule.