Skip to content

Cape Verde na safari ya ndoto Kombe la Dunia 2026

  • Makala

“SAFARI  ya Cape Verde ni ukumbusho kwamba shauku na umoja vinaweza kushinda changamoto”, alisema, Rais wa CAF, Patrice Motsepe, alipowapongeza kwa mafanikio hayo.

KWA kufuzu Kombe la Dunia 2026, Cape Verde, wamejiunga na orodha ya mataifa madogo yaliyoandika historia.

Ni Iceland pekee, yenye idadi ndogo kidogo ya watu, iliyowahi kufikia mafanikio kama hayo.

Cape Verde limefuzu kwa mara ya kwanza katika Kombe ka Dunia  2026  baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Eswatini siku ya Jumatatu.

Ushindi huo uliifanya kuwa taifa dogo la pili katika historia kufuzu kwenye michuano  hiyo mikubwa zaidi ya soka duniani.

Blue Sharks, kama wanavyojulikana, walipata mabao kupitia Dailon Livramento, Willy Semedo na Stopira katika mechi yao ya mwisho ya kufuzu. Ushindi huo uliwahakikishia tiketi yao ya kushiriki kipute hicho kitakachofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Baada ya kipindi cha kwanza kilichojaa taharuki, Cape Verde walirudi uwanjani wakiwa na ari ya kutimiza ndoto.

Nahodha wao Dailon Livramento alifungua ukurasa wa ushindi kwa bao safi kunako dakika ya 48, baada ya shambulizi la kasi lililovunja ngome ya Eswatini.

Dakika sita baadaye, Willy Semedo, aliongeza bao la pili kwa shuti kali kutoka nje ya boksi, hatua iliyowafanya mashabiki wa Cape Verde kusherehekea kwa shangwe visiwani kote.

Mchezaji mkongwe aliyeingia uwanjani dakika za mwisho, Stopira, alihakikisha ushindi huo kwa bao la tatu la muda wa nyongeza, akiwaletea furaha isiyoelezeka.

“Tumeota ndoto hii kwa miaka mingi. Ushindi huu ni kwa ajili ya kila raia wa Cape Verde, ndani na nje ya nchi”, alisema, Livramento, baada ya mechi.

Cape Verde walimaliza kileleni mwa kundi ‘D’ wakiwa na pointi 23 kutokana na mechi 10, wameshinda mara saba, wametoka sare mbili na wamepoteza moja pekee. Uthabiti wao umevutia mashabiki barani Afrika na duniani.

Katika mechi iliyotangulia, walitoka sare ya 3-3 dhidi ya Libya, na hivyo kulazimika kushinda dhidi ya Eswatini ili kuhakikisha kufuzu, jambo walilolifanya kwa kishindo.

Kocha Pedro Brito, anayesimamia timu hiyo tangu 2021, alisifu nidhamu na umoja wa wachezaji wake.

“Tunaweza kuwa taifa dogo, lakini, mioyo yetu ni mikubwa. Timu hii imeonyesha nguvu ya kuamini”, alisema, Brito, baada ya mechi.

Kwa kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026, Cape Verde wamejiunga na orodha ya mataifa madogo yaliyoandika historia.

Ni Iceland pekee, yenye idadi ndogo kidogo ya watu, iliyowahi kufikia mafanikio kama haya.

Wakiwa na idadi ya watu wapatao 600,000 pekee, Cape Verde sasa wanakuwa taifa dogo la pili kuwahi kushiriki Kombe la Dunia kwa wanaume.

“Hii ni ndoto iliyotimia. Soka limetuweka pamoja kama taifa”, alisema, shabiki Joao Lopes mjini Praia, ambako maelfu  ya watu walijitokeza usiku kucha kusherehekea.

Kutoka mji mkuu wa Praia hadi visiwa vya Sao Vicente na Sal, wananchi walijimwaga mitaani mara baada ya filimbi ya mwisho.

Gari zilipiga honi, muziki ulisikika mitaani na wachezaji wa zamani walishiriki sherehe.

Rais, Jose Maria Neves, alituma ujumbe wa pongezi kwa timu hiyo, akisema ushindi huo ni ‘ushindi wa imani, uvumilivu na umoja wa kitaifa”.

“Cape Verde imeonyesha ulimwengu kuwa hata mataifa madogo yanaweza kutimiza ndoto kubwa”, aliandika, kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii.

Watoto waliokuwa wakicheza kandanda mitaani walitaja  majina ya mashujaa wao wapya, Livramento, Semedo na Stopira.

Baada ya furaha hiyo, macho sasa yanaelekezwa katika maandalizi ya Kombe la Dunia 2026, ambako Cape Verde watakutana na mataifa makubwa ya soka duniani.

Kocha, Brito, alisema, wataendelea kubaki wanyenyekevu licha ya mafanikio hayo.

“Kufuzu ni mwanzo tu. Tunataka kwenda huko kupambana, si kushiriki pekee,‚Äù alisema kwa kujiamini.

Blue Sharks wanatarajiwa kuanza mechi za kirafiki mwishoni mwa mwaka huu ili kuimarisha mbinu zao kabla ya fainali hizo.

Cape Verde wamekuwa mfano wa matumaini barani Afrika. Miaka 20 iliyopita, walikuwa wakihangaika katika hatua za awali za kufuzu.

Lakini uwekezaji katika soka la vijana, makocha na miundombinu umeleta mabadiliko makubwa.

Sasa, wachezaji wao wengi wanacheza katika ligi kubwa za Ulaya, wakiiletea timu yao uzoefu na ubora wa hali ya juu.

Safari yao ni somo kwa mataifa mengine madogo barani Afrika kwamba bidii na umoja vinaweza kuzaa matunda.

Cape Verde wamaliza kileleni mwa kundi ‘D’ wakiwa na pointi 23 kutokana na mechi 10, wakiwaacha Simba Wasiofugika wa Cameroun, wakiwa hawaamini kwa tofauti ya pointi nne.

Cape Verde haikucheza soka ya kimataifa kwa karibu miaka 25 iliyopita, lakini, sasa inakwenda kwenye fainali za mwaka ujao huko Amerika Kaskazini ikiwa ni miongoni mwa wawakilishi tisa wa Afrika.

Wanaungana na Morocco, Tunisia, Misri, Algeria na Ghana ambazo tayari zimeshafuzu.