Skip to content

Ramaphosa asema usitishaji mapigano Gaza hauathiri kesi ya Israel ICJ

  • Afrika

CAPE TOWN, AFRIKA KUSINI

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amesema ingawa makubaliano ya hivi majuzi ya amani kuhusu Gaza yanakaribishwa, hayataathiri kesi ya nchi hiyo dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Rais aliyasema hayo alipokuwa akijibu maswali katika Baraza la Kitaifa la Mikoa Bungeni, Cape Town.

“Mkataba wa amani uliofikiwa, ambao tunaukaribisha, hautakuwa na uhusiano wowote na kesi iliyopo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Kesi inaendelea na sasa inabidi ifike hatua ambayo Israel inapaswa kujibu maombi yetu ambayo yamewasilishwa mahakamani na wanapaswa kufanya hivyo ifikapo Januari mwakani,” Ramaphosa aliiambia bunge.

Wakati Afrika Kusini ikikaribisha awamu ya kwanza ya amani, ikiwa ni pamoja na usitishaji vita na kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina, Ramaphosa alisema kwamba mwishowe, haki ya kweli lazima ipatikane kwa watu wa Palestina.

“Hatuwezi kwenda mbele bila uponyaji unaotakiwa kufanyika, ambao pia utatokana na kesi iliyoanzishwa kusikilizwa ipasavyo,” alisema.

Mnamo Disemba 2023, Afrika Kusini ilienda kwenye mahakama ya ICJ ikitaka amri ya kulazimisha Israeli kusitisha mashambulizi yake dhidi ya Palestina na kutangaza vitendo hivyo kama mauaji ya halaiki.

Mnamo Januari na Machi 2024, mahakama ilitoa hatua za muda, kuamuru Israeli kuhakikisha utoaji wa haraka wa chakula cha msingi huko Gaza.

Ramaphosa alisema kuwa, kama mshiriki wa kesi katika ICJ, Afrika Kusini haiwezi kulazimisha mahakama kuharakisha uamuzi wake, hata kama Israel inaendelea kukiuka hatua kadhaa za muda zilizoamriwa na ICJ.

Hata hivyo amesisitiza kuwa juhudi za kimataifa zinaendelea kukomesha vitendo haramu vya Israel huko Gaza na kuhakikisha uwajibikaji wa ukatili unaofanywa dhidi ya Wapalestina.

“Michakato hii inafanyika katika Umoja wa Mataifa kupitia Kundi la The Hague, ambalo ni jumuiya ya kimataifa yenye nia ya kutetea sheria za kimataifa na kutenda kwa mshikamano na watu wa Palestina,” Ramaphosa alisema.

“Serikali ya Afrika Kusini inasalia na nia thabiti ya kutumia kila njia inayopatikana ya kisheria na kidiplomasia kuwalinda watu wa Palestina na kuzingatia utawala wa sheria,” aliongeza.