Skip to content

Ajali ya moto kwenye kiwanda cha nguo waua watu 16

DHAKA, BANGLADESH

TAKRIBAN watu 16 wamefariki dunia baada ya moto mkubwa kuzuka katika kiwanda cha nguo nchini Bangladesh, huku maofisa wakionya kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka.

Miili 16 imepatikana lakini ilichomeka kiasi cha kutotambulika, shirika la zima moto limesema.

Jamaa waliofadhaika walikusanyika nje ya kiwanda cha ghorofa nne katika eneo la Mirpur huko Dhaka siku ya Jumanne kuwatafuta wapendwa wao ambao bado hawajapatikana.

Moto huo uliozuka katika kiwanda hicho majira ya saa sita mchana, ulizimwa baada ya saa tatu. Lakini ghala la kemikali lililo karibu liliendelea kuwaka, serikali imesema.

Mkurugenzi wa huduma ya zima moto, Mohammad Tajul Islam Chowdhury aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa waathiriwa walikufa “papo hapo” baada ya kuvuta “gesi yenye sumu kali.”

Polisi na maofisa wa kijeshi bado wanajaribu kuwatafuta wamiliki wa kiwanda na ghala hilo, Chowdhury aliwaambia wanahabari.

Uchunguzi kuhusu iwapo ghala hilo lilikuwa likifanya kazi kihalali pia unaendelea, aliongeza. Wanafamilia waliokuwa na machozi walisimama nje ya majengo yaliyokuwa yameungua, wengi wao wakiwa wameshikilia picha za jamaa zao waliopotea.