MGOMBEA wa uwakilishi jimbo la Kiwani, Hemed Suleiman Abdulla, amesema akichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo hilo atahakikisha anawawezesha wajasiriamali na vikundi vya ushirika katika kukuza biashara zao.
Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti akiwa katika muendelezo wa kampeni zake za kukutana na makundi maalum katika vijiji vya Mchakwe na Jombe kwa Sanani vilivyomo ndani ya jimbo la Kiwani.
Alisema akiwa mwakilishi wa Kiwani atahakikisha anawawezesha wajasiriamali na vikundi vya ushirikika kwa kuwapatia mitaji, mikopo isiyo na riba na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanyia shughuli zao na kujiendeleza kimaisha.
Hemed alisema atahakikisha anawapatia elimu na soko la uhakika wajasiriamali ambao watatoka ndani ya jimbo la kiwani ili kufanya biashara zao kisasa na kupata faida siku hadi siku.
Akizungumzia sekta ya michezo, Hemed aliwaahidi wanamichezo wa jimbo la Kiwani kuwa ataendelea kuwa pamoja nao kwa kuwapatia vifaa vyote muhimu vya kufanyia mazoezi na kuwaletea wakufunzi wa mazoezi ili kuwafundisha namna bora ya ufanyaji mazoezi kwa afya salama.
Kwa upande wa sekta ya elimu, mgombea uwakilishi jimbo la Kiwani aliaahidi kwa kushirikiana na viongozi wenzake watajenga skuli kubwa ya kisasa katika kijiji cha Mchakwe ambayo itawaondolea usumbufu wanafunzi wa kufuata skuli masafa ya mbali.
Alifahamisha kuwa jimbo la Kiwani limenufaika na ujenzi wa miundombinu ya barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami na kuwaahidi wananchi wa Mchakwe kuwajengea barabara ya Mchakwe ambayo itasaidia kufungua shughuli za kiuchumi jimboni humo.
Aidha, Hemed alisema kwa kutambua mchango wa vijana, atakapopata ridhaa ya kuwa mwakilishi wa jimbo hilo atasimamia upatikanaji wa ajira kwa vijana sambamba na kupatiwa nyenzo za kuwawezesha kujiajiri.
Sambamba na hayo alisema ataendelea kusimamia ulinzi na usalama ndani ya jimbo la Kiwani kwa kuwapatia vifaa vya kisasa polisi jamii ili kuendelea na kazi zao za ulinzi shirikishi jimboni humo.
Kwa upande wake, mgombea ubunge jimbo la Kiwani, Hija Hassan, alisema endapo atachaguliwa kuwa mbunge ataimaridha huduma za afya ikiwemo upatikanaji wa matibabu na vipimo bure na kuhakikisha mama wajawazito wanajifungulia ndani ya jimbo la Kiwani na kupatiwa huduma zote stahiki bila ya malipo.
Hija alisema watakapopewa ridhaa ya kuwa viongozi jimboni humo watawatatulia wazazi jukumu la kuchangia gharama za masomo katika skuli na madrasa zote zilizomo ndani ya jimboni la Kiwani ambapo jukumu hilo litatelelezwa na viongozi wa Jimbo hilo.
