KAMPALA,UGANDA

SHIRIKA la Afya Ulimwenguni (WHO) limeiagiza  Mamlaka ya Uwanja wa ndege wa kimataifa, Entebbe kufanya uchunguzi wa  Ebola wa lazima kwa abiria wote wanaoingia Uganda kupitia uwanja huo.

Taarifa ziliopo zimeeleza kwamba,  mamlaka ya uwanja wa ndege imekuwa ikiwachunguza abiria wanaotokea Jamuhuri la Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako ugonjwa huo umeua watu 370.

Hata hivyo kwa mujibu wa  Simon Ebachu, Mkuu wa kitengo cha uchunguzi wa  Ebola kutoka  WHO, abiria wote wanaoingia nchini humo wanapaswa kuchunguzwa.

Uchunguzi wa lazima umekuja wakati DRC ikipambana na  Ebola ambayo iliibuka Agosti mwaka jana katika Jimbo la Kivu Kaskazini , mpakani na Uganda.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka wizara ya Afya DRC, takriban watu  400 wameambukizwa virusi vya  Ebola.

Ili kuwezesha uchunguzi huo, kwa mujibu wa Ebachu, zaidi ya wafanyakazi wa afya  40 wamewekwa katika uwanja wa ndege kuwachunguza abiria.

Ebachu alisema abiria watachunguzwa kwa kutumia kifaa maalumu ambacho kitapima joto lao la mwili mara watakapowasili uwanjani hapo.

MAONI YAKO