KHARTOUM,SUDAN

MAKAMU  Mwenyekiti wa Chama cha Umma cha nchini Sudan ametoa hati maalumu ya kisiasa yenye mapendekezo ya kuivua nchi hiyo kutokana na mgogoro wa hivi sasa na kuiepusha kutumbukia kwenye vita vya ndani.

Bi Maryam Sadiq al Mahdi amesisitiza kuwa, miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuundwa serikali ya mpito kwa muda maalumu ambayo itasimamia mabadiliko yanayopinganiwa na wananchi.

Hii ni katika hali ambayo,  Jumapili, serikali ya Sudan ilisema kuwa, watu 24 wameshauawa katika maandamano ya nchi nzima yanayoendelea hivi sasa nchini humo kulalamikia ughali wa maisha.

Wakati serikali ya Sudan ikidai kuwa ni watu 24 waliouawa hadi hivi sasa, Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema kuwa watu wasiopungua 40 wameshauawa katika maandamano hayo yaliyoanza tarehe 19 Disemba 2018, wakiwemo watoto wadogo na maafisa wa kutoa misaada.

Wakati huohuo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi Kusini mwa Afrika, SADC, imetoa wito kwa viongozi wote wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuzingatia majadiliano na kuunda serikali ya muungano.

Mwenyekiti wa SADC Edgar Lungu ametoa wito huo kutokana na hofu ya kuzuka machafuko katika Jamhuri hiyo. Lungu amesema serikali za muungano zimefanikiwa katika nchi kadhaa za Afrika kama Afrika Kusini, Zimbabwe na Kenya.

Amesema pia tayari amezungumza na Feliy Tshisekedi aliyetajwa mshindi wa uchaguzi huo pamoja na washikadau wengine wakiwemo wale walioko katika maeneo ya Maziwa Makuu. Kulingana na Lungu jumuiya ya SADC imezingatia mashaka yaliyotolewa na Kanisa Katoliki nchini Congo ambalo lilikuwa na waangalizi zaidi ya 40,000 katika uchaguzi huo.

Mapema Ijumaa tume ya uchaguzi ilimtangaza Tshisekedi kama aliyeshinda kwa asilimia 38.57 ya kura. Mpinzani wake Martin Fayulu amewasilisha rufaa katika mahakama ya katiba mjini Kinshasa akisema matokeo ya kura hiyo yalikuwa yamechakachuliwa.

MAONI YAKO