ABDI SHAMNAH, IKULU

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Omar Hassan ‘King’amesema tayari wizara  hiyo imekipatia kikundi cha Taarabu cha taifa ofisi za kuendeshea shughuli zake pamoja na kuwa na bajeti ili kukidhi mahitaji ya msingi.

Alisema pamoja na mambo mengine, wizara imetekeleza kikamilifu maagizo ya serikali ili kukiwezesha kikundi hicho kufanya shughuli zake kwa ufanisi pamoja na kuleta ustawi bora wa wasanii wanaokitumikia.

Kingi, alisema hayo juzi katika uwanja wa kufurahishia watoto Tibirinzi Chake-chake Pemba, katika taarabu maalum iliyoandaliwa, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 55 ya mapinduzi ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alikuwa mgeni rasmi katika taarabu hiyo, ambapo mamia ya wananchi kutoka mikoa yote ya Zanzibar walijumuika na kukonga nyonyo zao vilivyo.

Akitoa taarifa za utekelezaji wa maagizo hayo, alisema tayari wasanii wa kikundi hicho wameanza kupokea mirahaba kutokana na nyimbo nne kati ya 12 walizozisajili pamoja na kujiingizia mapato kutokana na ushirikiano uliopo kati ya kikundi hicho  na baadhi ya taasisi, kama vile ZSTC.

Katika hafla hiyo, kikundi hicho kilicho chini ya mwenyekiti  msanii nguli Idd Suweid, kiliibuka na nyimbo kadhaa, zikiwemo zile zenye mnasaba na mapinduzi, ambapo magwiji wa sanaa hiyo walighani na kukonga vilivyo nyonyo za watazamaji/wasikilizaji.

Miongoni mwa nyimbo zilizonogesha usiku huo  ni pamoja na miaka 55 ya Mapinduz iliyoimbwa na Pro. Gogo, anaetoa ni Mola iliyoghaniwa na al-anisa Sada Mohamed,‘tarehe 11 (Idd Siweid), Ni yeye pamoja na umewashuka iliyoimbwa an al-anisa Amina Ramadhan.

Nyengine ni Wahoi, Njoo kwa mtu mkweli (al-anisa Rukia Ramadhan), maisha ya Vijijini iliyoghaniwa na chiriku Hilda Mohamed, mpewa hapokonyek ,kama kupenda ni dhara iliyoimbwa na sauti ya Zege Makame Faki pamoja na ninae iliyoghaniwa vyema na mpendwa na wengi Idd Suweid.

Kikundi cha Taarabu cha Taifa kina jumla ya wasanii 35 wanaotoka katika vikundi saba vya taarabu hapa Zanzibar.

MAONI YAKO