NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

MICHUANO ya 13 ya kombe la mapinduzi imefikia tamati jana na timu ya  Azam kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfulululizo, baada ya  kuifunga Simba mabao 2-1, mchezo uliopigwa uwanja wa Gombani Pemba.

Katika mchezo huo ambao ulihudhuriwa na mashabiki wengi kutoka maeneo mbali mbali ya kisiwa cha Pemba, Azam ambayo imeshusha kikosi kamali tofauti na Simba, hakikuwa na kikosi kamili kutokana na kukabiliwa na michezo ya kimataifa.

Simba ilianza pambano kwa kasi kubwa na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini walishindwa kuzitumia vyema na kushindwa kupata bao.

Azam ilizinduka katika dakika 20 za mwisho kuelekea katika mapumziko na walifanikiwa kupata bao daakika ya 44 lililofungwa na Mudathir Yahya kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Simba Ali Salim bao ambalo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili Simba walianza kwa kulishambulia lango la Azam wakitafuta bao la kusawazisha, ambapo juhudi hizo zilifanikiwa katika dakika ya 64 baada ya beki Yussuf Mlipili kuisawazisha kwa kichwa akiunganisha kona ya Shiza Kichuya.

Baada ya bao hilo mchezo huo uliendelea kuwa wa kushambuliana kwa zamu kila mmoja akisaka bao la ushindi, lakini Azam walifanikiwa kupata bao la pili dakika ya 72 lililofungwa Obrey Chirwa baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Nicolas Wadada.

Baada ya bao hilo timu zote zilicheza kwa kasi kubwa Simba wakitafuta bao la kusawazisha, Azam wakitaka kuongeza idadi ya mabao, lakini dakika 90 zinamalizika Azam ikifanikiwa kutoka na ushindi wa mabao 2-1.

Huu ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Azam katika fainali za kombe la mapinduzi hivyo kwa kutokana na ushindi huo ,Azam wanakabidhiwa rasmi kombe hilo kuwa mali yao.

Kwa ushindi huo Azam wanapewa kombe na kujizolea kitita cha shilingi milioni 15 na medali za dhahabu, huku Simba wakijizolea kitita cha shilingi milioni 10 na medali za fedha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikuwa mgeni rasmi katika fainali hiyo.

MAONI YAKO