ANKARA,UTURUKI

WAPELELEZI  wa Uturuki wamefutilia mbali shughuli nyingine ya upekuzi katika Ubalozi Mdogo wa Saudi Arabia jijini Istanbul iliyolenga kubainisha kilichomsibu mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi.

Khashoggi ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudi Arabia hajajulikana alipo tangu kuingia kwenye ubalozi huo tarehe 2 mwezi Oktoba mwaka huu. Mamlaka za Uturuki zinakisia kuwa huenda aliuawa kwenye ubalozi huo.

Shughuli ya upekuzi ilitarajiwa kuanza  Jumanne usiku kwa saa za nchi hiyo. Lakini vyombo vya habari nchini Uturuki vinaripoti kuwa wapelelezi walifutilia mbali mpango huo dakika za mwisho baada ya Saudi Arabia kukosa kushirikiana nao.

Shughuli ya upekuzi iliyoendeshwa na wapelelezi wa Uturuki na Saudi Arabia na iliyodumu usiku kucha ilimalizika mapema juzi  Jumanne.

Awali, vyombo vya habari nchini Uturuki viliripoti kuwa mkuu wa ubalozi mdogo wa Saudi Arabia alirejea nchini mwake  Jumanne.

Aidha Saudi Arabia imekanusha madai kuwa mwanahabari huyo aliuawa kwenye ubalozi huo.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kuwa maafisa wa Saudi Arabia wanapanga kusema kuwa Khashoggi alifariki kwenye ubalozi huo wakati wa mahojiano yaliyokwenda mrama.

MAONI YAKO