RIO DE JANEIRO, BRAZIL

Polisi nchini Brazil wanapendekeza katika kesi mpya kwamba Rais Michel Temer afikishwe mahakamani kwa ajili ya ufisadi, uhalifu wa kifedha na kujihusisha na uhalifu.

Ripoti hiyo ya polisi iliyopatikana na shirika la habari la Associated Press iliwasilishwa katika mahakama ya juu ya nchi hiyo hapo jana.

Mkuu wa sheria wa Brazil atakuwa na siku 15 kuamua iwapo aifuatilie kesi hiyo.

Bunge la nchi hiyo pia litalazimika kupiga kura ili kukubali kesi hiyo iendelee jambo litakalousimamisha kwa muda uongozi wa Temer ambaye muhula wake unakamilika Desemba 31.

Wabunge walikataa kupiga kura katika madai ya awali ya ufisadi dhidi ya Temer.

Ripoti hiyo ya polisi inasema rais huyo anashukiwa kupokea hongo ili kuzipendelea kampuni za usimamizi wa bandari kupitia kwa mamlaka ya rais.

Wakili wake lakini anasema Temer bado hajaiona ripoti hiyo.

MAONI YAKO