MKAAZI wa Matemwe Mbuyutende, Juma Ujudi Ali akizungumza na waandishi wa habari akiishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwaruhusu kutumia maeneo yao ya makaburi kwa ajili ya kuzikana sambamba na kuruhusiwa kulitumia eneo lao la bandari. (PICHA NA ABDALLA MASANGU).

Na Mwandishi Wetu

WANANCHI wa kijiji cha Matemwe Mbuyutende Mkoa wa Kaskazini Unguja, wamehimiza kutekelezwa kwa amri ya serikali kutaka mwekezaji aliyebomoa ukuta wa eneo lao la makaburi, aujenge upya.

Itakumbukwa kuwa, Julai 22, 2018, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, alitembelea eneo hilo kutafuta suluhu ya mzozo ulioibuka kati ya wanakijiji na mmoja wa wawekezaji wa sekta ya utalii, aliyedai kuuziwa eneo hilo.

Balozi Seif aliongoza kamati iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kutafuta suluhu ya mzozo huo unaohusu eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2.9.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na mawaziri wenye dhamana ya fedha, utalii na ardhi, pamoja na watendaji wa mamlaka nyengine, Balozi Seif aliagiza eneo hilo liendelee kutumika kwa ajili ya kuzikia.

Hata hivyo, pamoja na maamuzi hayo ya serikali, inaonekana joto la wananchi wa kijiji hicho bado halijashuka, kama walivyoshuhudiwa na waandishi wa habari waliofika huko mwishoni mwa wiki kutokana na kutotekelezwa kwa amri ya kuujenga ukuta unaozunguka eneo hilo.

Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wenzao, baadhi ya wanakijiji, walieleza kushangazwa kwao, kwamba hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kuujenga ukuta huo ambao awali walidai ulivunjwa na mwekezaji anayekusudia kulitumia eneo hilo kwa mradi wa hoteli.

Mzani Ussi Haji, alisema kwa vile serikali ilishatoa uamuzi kuhusiana na eneo hilo, ni lazima agizo hilo liheshimiwe na kuwaachia wananchi waendelee kulitumia kwa shughuli za mazishi.

Mbali na hilo, alisisitiza kuwa ukuta wa eneo hilo ujengwe upya kwa urefu wa kati ya mita sita na saba kwenda juu ili makaburi yapate hifadhi ya uhakika.

Ussi alifahamisha kuwa, mbali na hilo, katika maamuzi ya utatuzi wa mgogoro huo, serikali ilielekeza mipaka ya eneo la makaburi na ufukwe ibakie kama ilivyo ili iendelee kutumika kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa kijiji hicho pamoja na wawekezaji.

Mwanakijiji mwengine, Ayesha Haji Ali, alisema eneo hilo limekuwa likitumiwa kwa kuzikiana kwa miaka mingi sasa kabla serikali haijaja na sera ya uwekezaji katika sekta ya utalii, na kwamba ufukwe uko huru kwa wavuvi.

MAONI YAKO