NA NASRA MANZI
JUMLA ya viongozi na wachezaji 34 wa kikosi cha Yanga, wanatarajiwa kuwasili visiwani hapa kesho kwa ajili ya kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Malindi utakaopigwa Oktoba 13 kwenye uwanja wa Amaan.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Yanga na Malindi, Yahya Juma Ali wakati akizungumza na wandishi wa habari jana.
Alisema lengo kuu la mchezo huo ni kumuaga nahodha wa timu hiyo, Haroub Nadir ‘Cannavaro’ sambamba na kumpongeza kwa kupewa nafasi ya umeneja wa timu hiyo kwa kumuamini baada ya kustaafu ili kupeleka mbele maendeleo ya Yanga.

Alisema, mchezo huo utakuwa wenye usalama kwa kuhakikisha ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa timu pamoja na mashabiki watakaohudhuria mchezo huo.
“Suala la ulinzi litakuwa katika hali ya juu kwa vile mchezo sio uhasama bali kujenga urafiki, umoja na mshikamano”, alisema.
Pia alisema timu hiyo itacheza mchezo mmoja pekee na itakuwa ikifanya mazoezi yake katika uwanja wa Fuoni, Ngome kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Hivyo, alitoa wito kwa vijana kujielewa katika michezo na kutambua kuwa michezo ni ajira,hivyo ni vyema kuzitumia fursa hizo.

Viingilio vya mchezo huo itakuwa (VIP 5,000 ), (Urusi 2,000) na Wings itakuwa shilingi 3,000, hivyo aliwataka mashabiki kujitokeza kwa ili kuwaunga mkono vijana katika michezo.

MAONI YAKO