NA MWAJUMA JUMA
MTIHANI wa utimamu wa waamuzi ‘Copa Test’, unarajiwa kufanyika kesho katika uwanja wa Amaan mjini hapa.

Mtihani huo utakwenda sambamba na mafunzo ya siku mbili ya darasani ya waamuzi kupitia sheria 17 za soka, unafanyika kwa ajili ya msimu mpya wa ligi utakaoanza Oktoba 20 mwaka huu.

Kabla ya kufanyika kwa mtihani huo, leo asubuhi kutakuwa na zoezi la kupimwa afya kwa waamuzi wote ambao watashiriki mtihani huo .

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu wa Kamati ya Waamuzi Zanzibar, Muhsin Ali Kamara, alisema, awali mtihani huo ulikuwa fanyike jana, lakini, umesogezwa mbele kutokana na tatizo la uwanja.

Alisema kuwa mtihani huo utawajumuisha waamuzi 40 wakiwemo 12 kutoka Pemba utafanyika kuanzia majira ya saa 1:00 za asubuhi.

Alisema kuwa waamuzi ambao watafaulu ndio watakaochezesha Ligi Kuu ya Zanzibar na watakaofeli watawapa muda wa miezi mitatu kujiandaa ili kuweza kuchezesha ligi.
Hata hivyo, alisema, katika mtihani huo watatoa waamuzi ambao watawapumzisha kutokana na umri wao kuonekana kupita.

Aidha, alisema, mtihani huo utasimamiwa na ZFA wenyewe na hakuna mkufunzi kutoka nje kwa vile hii ni ligi yao ya ndani na wapo watu ambao wamepata mafunzo kwa ajili hiyo.

MAONI YAKO