NA KHAMIS AMANI
MRAJIS wa Chama cha Michezo Zanzibar, ameburuzwa mahakama kuu ya Zanzibar, kuzuwiwa kufanyika kwa uchaguzi katika klabu ya soka Malindi iliyopo wilaya ya Mjini Unguja.

Lakini hata hivyo, kwa mujibu wa wadai wa kesi hiyo uchaguzi huo tayari umeshafanyika, hivyo mahakama hiyo iliyo chini ya Jaji Abdulhakim Ameir Issa, imeutaka upande huo kubadilisha madai yao.

Mbali ya Mrajis wa Chama cha Michezo, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ya madai ni Mohammed Aljabri pamoja na Mohammed Massoud Rashid.

Wadai katika kesi hiyo ni Mtumwa Said Haji pamoja na Ali Salum Mkweche, ambao kwa pamoja wamewasilisha madai yao mahakamani hapo ya kuzuwia kufanyika kwa uchaguzi katika klabu hiyo.

Wakiwa mahakamani hapo juzi mbele ya Jaji Abdulhakim, wakati kesi hiyo ilipofikishwa kwa ajili ya kutajwa, Jaji huyo aliuhoji upande wa wadai kuhususiana na uchaguzi huo na kudai tayari umeshafanyika.

Hivyo kutokana na hali hiyo, Jaji Abdulhakim Ameir Issa, ameutaka upande huo wa wadai kubadilisha maombi yao juu ya kesi hiyo na kuiahirisha hadi Oktoba 25 mwaka huu kwa kutajwa, ili kutoa nafasi kwa upande wa wadai kubadilisha maombi yao.

MAONI YAKO