NA NIZAR KARIM VISRAM, DAR ES SALAAM

BARAZA kuu la Umoja wa Mataifa (UN) lilikuwa na mkutano wake wa kilele jijini New York kuanzia Septemba 25 hadi Oktoba 1, mkutano huu hufanyika kila mwaka na huhudhuriwa na marais au wawakilishi wao kutoka nchi wanachama wa UN.

Katika mkutano huo kila kiongozi hupewa nafasi ya kuzungumza na kueleza maoni na sera za nchi zao.

Rais Donald Trump wa Marekani alipangwa awe wa pili kutoa hotuba yake akitanguliwa na rais wa Brazil. Lakini zamu yake ilipofika hakuonekana.

Nafasi yake ikalazimika apewe msemaji wa tatu aliyepangwa kuzungumza kwenye hadahra hiyo ambaye ni rais Lenin Moreno wa Ecuador ambaye alikuwa katika kiti cha magurudumu.

Wakati Lenin anazungumza ndipo msafara wa Trump uliwasili, naye akapewa nafasi ya tatu, hakukuwa na maelezo ya kuchelewa wala msamaha alioutoa.

Hata hivyo katika vyombo vya habari hotuba ya Trump ilipewa uzito zaidi, sio tu kwa sababau anaongoza taifa la kibabe duniani, bali kutokana na yale aliyoyasema.

Matamshi yake yaliwafanya wakuu wa dunia kuangusha vicheko. Walicheka  wakati Trump alipodai kuwa utawala wake umepata mafanikio makubwa ambayo hayajapata kutokea chini ya rais yeyote mwengine nchini Marekani.

Maneno kama haya huwa anayatamka mbele ya wafuasi wake nchini Marekani, nao huwa wanamshangilia, lakini mkutano wa UN hali ilikuwa ni tofauti.

Hawakucheka kwa sababu walikuwa wamefurahishwa na majigambo yake, kwani kuna mengi aliyoyasema ambayo yaliwasikitisha wengi wao.

Alitoa vitisho dhidi ya Iran, Venezuela na Syria. Kisha akatangaza vita vya kibiashara dhidi ya China, Urusi na nchi nyingine. Kama hiyo haitoshi akaishambulia Ujerumani.

Wakati Trump akiishambulia Ujerumani, wajumbe wa taifa hilo kwenye mkutano huo, walionekana wakitikisa vichwa hasa pale Trump aliposema nchi hiyo imekuwa mtumwa wa gesi kutoka Urusi.   

Akazisifu Israel na Saudi Arabia akisema nchi hizo ni za kupigiwa mfano. Akamsifu mkuu wa Korea Kaskazini (DPRK) Kim Jong-Un na kusema mkuu huyo amemwandikia barua nzuri sana kwa sababu wanapendana.

Katika mkutano kama huo mwaka mmoja uliopita, Trump huyu huyo alimtisha Kim Jong-Un pale aliposema atammaliza yeye na nchi yake yote, mwaka huu amezigeukia Iran, Venezuela na China.

Pia ameishambulia UN na kusema nchi yake haina imani katika ushirikiano wa kimataifa (multilateralism), bali itashirikiana na nchi moja moja (bilateralism). Amezitaka nchi zote duniani nazo zifanye hivyo. Wajumbe wakapigwa na bumbuwazi.

Akasema: “Nitaheshimu uhuru wa kila nchi bila ya kuingilia uhuru wa kujiamulia mambo yao”.

Hata hivyo Marekani ina historia refu ya kutumia majeshi yake kupindua tawala za nchi nyingi duniani. Pia imeeneza majeshi e katika makontinenti yote. Halafu Trump anasema hataingilia mambo ya ndani.

Trump alisema Iran inachochea vita kwa hivyo ameamua kuongeza vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Akasema viongozi wa Iran “wanaiba mabilioni ya dola na kujitajirisha”.

Akadai kwa vile Iran ina mpango wa kuunda makombora na silaha za nyuklia, hivyo amejitoa kutoka mkataba wa kimataifa wa kuzuia uundaji wa silaha za nyuklia nchini Iran (JCPOA).Trump pia amezitaka nchi zote ziache kufanya biashara na Iran.

Hata hivyo, wengi hawakubaliani naye. Ujerumani kwa mfano imeiuzia Iran bidhaa za dola bilioni 117 mwaka jana. Ndio maana nchi za Ulaya zilikutana na kutamka kuwa zitaendelea kuunga mkono JCPOA na kufanya biashara na Iran. Ili kuepukana na kibano cha Marekani nchi hizo zimeamua kutumia sarafu ya Euro badala ya dola.

China nayo inaongoza katika kufanya biashara na Iran ikifuatiwa na Umoja wa Ulaya (EU). China inanunua mapipa 700,000 ya mafuta kutoka Iran kila siku. China pia ina miradi mingi ya ujenzi nchini Iran.

Uturuki na India nazo zimeonesha nia ya kuendelea kununua mafuta kutoka Iran. Japan, Ufaransa na Korea Kusini nazo zinafanya hivyo hivyo.

Ni dhahiri kuwa vikwazo vya Marekani haviungwi mkono na nchi nyingi ambazo pia zinaendelea kuheshimu JCPOA. Msimamo huu umechukuliwa siyo tu na nchi za Ulaya kama Uingereza na Ufaransa, bali pia na nchi ndogo kama Peru, Ivory Coast na Khazakstan.

Si ajabu kuwa asasi ya Marekani inayoshughulikia amani ulimwenguni (Carnegie Endowment for International Peace) imesema inasikitishwa Trump amejitenga mwenyewe badala ya kuitenga Iran katika uwanja wa kimataifa.

Sasa suala zima limefikishwa na Iran katika mahakama ya kimataifa (ICJ). Ni kwa sababu ICPOA ni mkataba wa kimataifa uliopitishwa na UN na kuridhiwa na Marekani. Nchi hiyo kwa hiyo inahalifu sheria ya kimataifa inapokataa kuitekeleza.

Iran imeitekeleza ICPOA kwa kuwaruhusu wachunguzi wa kimataifa kutoka shirika la nyuklia ulimwenguni (IAEA) kuja kuhakiki kuwa Iran haina mpango wa kuunda silaha ya nyuklia. Ni Israel ndio yenye silaha hizo ambazo imezificha na inakataa kuruhusu wachunguzi.

Trump pia alidai kuwa ni yeye ndiye aliyefanikisha kufukuzwa kwa wapiganaji wa ISIS nchi Iraq na Syria. Lakini ulimwengu unatambua kuwa huko Syria wapiganaji hawa wamefurushwa kwa msaada wa Urusi, Iran na Hezbollah.

Sasa kwa kufanya hivyo Marekani imetamka wazi nia yake ya kuupindua utawala wa Iran. Wakati huo huo Trump amedai eti Rais Hassan Rouhani wa Iran ameomba kukutana naye, akiongeza kuwa Rouhani ni “mtu mzuri sana”.

Rouhani alipoulizwa na wanahabari alisema yeye hajawahi kuomba kuonana na Trump bali ni Trump ndie aliyeomba mara nane kuonana naye. Akasema haoni umuhimu wa kuonana na Trump kwa muda huu.

Trump alimshambulia Rais Nicolás Maduro wa Venezuela akisema ni fisadi na kuwa ana nia ya kuongeza vikwazo dhidi ya utawala wake. Akasema atachukua hatua stahiki dhidi ya Venezuela. Wachambuzi wanasema ana maana ya hatua za kijeshi.

Maduro katika hotuba yake alisisitiza haki ya wananchi wa Venezuela kujiamulia mustakbali wa nchi yao bila ya kuingiliwa. Akakutana na katibu mkuu wa UN, Antonio Guterres na akatoa mwaliko kwa mkuu wa haki za binadamu wa UN atembelee Venezuela.

Baada ya kumaliza hotuba yake Maduro akatembelea kanisa la Riverside lililo katika kitongoji cha Harlem jijini New York, wanakoishi Wamarekani weusi. Huko akaungana na Rais wa Cuba Bw Miguel Díaz-Canel nao wakapokelewa na wananchi 3,000.

Kiongozi mwengine kutoka Amerika Kusini aliyehutubia mkutano wa UN alikuwa Rais Evo Morales wa Bolivia. Yeye alimsomea Trump orodha ya nchi zilizowahi kushambuliwa kijeshi na Marekani.  

Akaongeza kuwa dikteta wa kweli ni Marekani ambayo imeeneza majeshi yake duniani kote. Akasema Marekani haina mapenzi na demokrasia wala haki za binadamu na ndio maana inapuuza sheria ya kimataifa na ushirikiano wa kimataifa na badala yake inashambulia nchi za kigeni.

Trump aliishambulia China kuwa inaingilia mambo ya ndani ya Marekani hasa kuhusu uchaguzi mdogo utakaofanyika mwezi ujao. Alisema China isingependa chama cha Trump kishinde kwa hiyo inapigia kampeni chama cha Democratic, lakini hakutoa ushahidi dhidi ya madai hayo.

Alisema China haimpendi kwa sababu yeye amekuwa akipambana na nchi hiyo katika ushindani wa biashara na amekuwa akishinda.

Trump akajibiwa na waziri wa China wa mambo ya nje Wang Yi. Katika hotuba yake alitamka kuwa siku zote China imekuwa ikifuata sera ya kutoingilia mambo ya ndani ya ncho yoyote. Kwa hivyo akakanusha vikali lawama za Trump zisizo na msingi.

Tanzania nayo hakubaki nyuma, kwani Rais John Magufuli aliwakilishwa na waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa Afrika mashariki, Dk. Augustine Mahiga. Yeye alitamka kuwa Tanzania inaamini katika ushirikiano wa kimataifa ili kupambana dhidi ya ugaidi, dawa za kulevya, umasikini na mabadiliko ya tabia nchi.

Akaongeza Tanzania inasikitisha kuona asasi za kimataifa kama shirika la biashara (WTO) na mkataba wa kuhifadhi mazingira vinadhoofishwa.

Pia akakumbusha haja ya kuleta mageuzi katika mfumo wa baraza la usalama la UN ili haki itendeke kwa nchi zote. Akataka mazungumzo ya kuleta mabadiliko hayo yaliyositishwa yaendelee. Akatoa wito pia kwa Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Cuba vilivyowekwa na rais Trump.

Waziri Mahiga pia akataka migogoro ya Sahara magharibi na Palestina itafutiwe ufumbuzi wa kudumu. Wapalestina alisema wanastahili uhuru wao na akatumai kuwa “uwezo na ubunifu” wa Israel na busara ya Wapalestina vitatumika.

Wengine wangesema ni “uwezo na ubunifu” huo wa Israel ndio ulioifanya nchi hiyo ipuuze na kudharau sheria ya kimataifa na maazimio ya UN tangu 1948.

0658-010308

nizar1941@gmail.com 

MAONI YAKO