KATIKA toleo letu la jana, tulichapisha habari juu ya Kampuni ya Ujenzi ya Kin Investment LTD ya Chake Chake, kukabidhiwa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo wa Kishindeni uliopo wilaya ya Micheweni Pemba.

Ujenzi wa uwanja huo ni muendelezo wa azma ya Rais wa Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein ya kujenga viwanja 11 katika wilaya za Unguja na Pemba kwa ajili kuhamasisha vuguvugu la kuibua vipaji vya wachezaji vilivyosheni ndani ya mawilaya.

Kwa mara nyengine, tunachukua nafasi hii kuipongeza serikali kwa azma yake hiyo ambayo katika hatua ya awali, imepanga kujenga viwanja vitano ili kuwarahisishia wananchi wakiwemo vijana kufanya mazoezi sambamba na kufikia hatua ya maendeleo kwenye sekta hiyo.

Bila ya shaka ni uamuzi unaokwenda sambamba na malengo ya kuona sekta ya michezo inazidi kupiga hatua huku pia ikitajwa kama sehemu inayoweza kutoa ajira kwa vijana wengi ikiwa kutakuwepo na mipango inayoendana na hilo.

Hivyo, tunachokiamini ni kwamba kukamilika kwa uwanja huo ni dhahiri itakuwa fursa kubwa kwa wananchi wa Micheweni hasa vijana kujitoa kwa ajili ya kushiriki michezo mbali mbali ndani ya wilaya hiyo.

Kubwa tunalopenda kuwambia wanamichezo na wananchi wa Micheweni ni kuhakikisha wanakuwa wasimamizi na walinzi wa mali za uwanja huo, ili uweze kukamilika kwa wakati sambamba na wakandarasi kujenga kwa kiwango cha hali ya juu.

Kwa kipindi kirefu, wilaya zetu zimekuwa zikikosa viwanja vyenye hadhi hali ambayo inatajwa kudumisha michezo hasa vijijini ambako huko ndiko kwenye chimbuko la vipaji mbalimbali vya michezo.

Hivyo, azma ya serikali ya kujenga viwanja hivyo vinavyotarajiwa pia kuwekewa mazingira mazuri ikiwemo uwekaji wa taa na nyasi bandia ili kuvifanya viwe vya kisasa ni hatua ya kupongezwa na kuungwa mkono na kila mmoja wetu.

Tutakapofanikiwa kujenga viwanja vya kisasa katika maeneo ya vijiji vyetu, tunaweza kuwavutia wawekezaji hasa katika maeneo yenye ustawi wa kiutalii kuanzisha au kudhamini timu na kutoa ajira kwa vijana katika maeneo hayo.

Wengi wetu bado tunakumbuka jinsi Nungwi ilivyokuwa imenawirishwa na timu za Mundu na Sharp Boys kwenye miaka ya nyuma kutokana na uungwaji mkono kwao na wawekezaji wa sekta ya utalii ndani ya kijiji hicho.

Kwa maana hiyo, kinachohitajika sasa ni ubunifu tu wa namna tutakavyoweza kuwashawishi wawekezaji kujiingiza moja kwenye sekta ya michezo baada ya kujengwa kwa miundombinu bora ya michezo vijijini.

Kama inavyofahamika namna michezo hivi sasa ilivyobiashara kubwa na nzuri, hivyo, tunachotakiwa ni kujitambua huku tukiwa na kila sababu kwa klabu zetu kuwa na malengo ya kuwekeza zaidi kimichezo.

Sasa lazima tufikie mahali na kuweka mikakati ya kweli katika kuzishajiisha klabu kuwa na malengo chanya ambayo yataziondoa katika utendaji wa mazoea na kuingia kwenye hatua ya maendeleo.

Ni imani yetu kwamba kuimarisha sekta ya michezo ni kuwajenga wananchi kuwa na afya bora, lakini, pia ni katika kubuni njia za ajira kwa vijana.

Hivyo sasa ni wakati kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya vijijini kujiandaa na kuipokea azma hiyo ya serikali katika kuona michezo ikipiga hatua zaidi kwa manufaa ya wanamichezo na taifa kwa ujumla.

Lakini pia tungelipenda kuchukua fursa hii kuwashauri viongozi wetu wa majimbo wakiwemo Wawakilishi na Wabunge kujitokeza kuunga mkono hatua hizo za serikali katika kufanikisha azma hiyo ya ujenzi wa viwanja wilayani.

Kwa vile nyinyi ndiyo wawakilishi wa wananchi, mtakuwa na kila sababu ya kusimamia hilo kwa hali na mali huku mkielewa wananchi wapo nyuma yenu.
Hongeza serikali kwa azma ya kujenga viwanja vijijini na kuinua sekta ya michezo.

MAONI YAKO