NA NIZAR KARIM VISRAM, DAR ES SALAAM

BUNGE la Canada limepitisha azimio likiwashutumu watawala wa Myanmar (zamani Burma) kwa uhalifu dhidi ya binadamu. Azimio lilipita bila ya kupingwa.

Canada imechukua hatua hii baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kutoa ripoti yake ikisema nchini Myanmar kumekuweko na mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya kabila la Rohingya na likitaka wakuu wa jeshi la Myanmar washitakiwe katika mahakama ya kimataifa ya jinai (ICC) iliyo jijini Hague.

Wabunge wa Canada wamekubaliana na ripoti hiyo ya UN iliyotolewa baada ya uchunguzi. Wametaka baraza la usalama la UN lifungue kesi katika mahakama ya ICC dhidi ya makamanda wa Myanmar. Kwa mujibu wa ripoti ya UN majenerali wa Myanmar wamehusika moja kwa moja katika mauaji haya ya halaiki.

Ripoti ya UN iliyotangazwa mwezi Agosti mwaka huu ina kurasa 444. Ni matokeo ya tume ya uchunguzi (UN Fact-Finding Mission on Myanmar– FFM). Ni tume ya wataalamu iliyoteuliwa na baraza la haki za binadamu la UN.

Inamtaja mkuu wa majeshi ya Myanmar pamoja na majenerali wenzake watano. Hawa wanashutumiwa kwa kuhusika katika mauaji katika jimbo la kaskazini la Rakhine na maeneo mengine. 

UN pia inamlaumu mkuu wa serikali ya Myanmar Bi Aung San Suu Kyi kwa kushindwa kuzuia mauaji.

Cha msingi ni kuwa UN sasa inakubali kuwa nchini Myanmar kumekuweko na mauaji ya halaiki yanaayoendeshwa na majeshi, kikosi cha usalama na wanamgambo wa jamii ya Kibudha ambao ndio walio wengi nchini Myanmar.

Udhalilishaji wa Warohingya ulianza miengo kadha iliyopita na mauaji yalianza mwaka 2012 wakati watu kiasi cha 100,000 walifukuzwa kutoka vijijini mwao na kulazimishwa kuishi katika kambi mithali ya wafungwa.

Na mwaka 2013 zaidi ya 140,000 wakafukuzwa. Miaka iliofuata idadi hii ikaongezeka.

Mauaji ya halaiki yalifikia kilele Agosti 2017. Katika muda mfupi wa miezi sita takriban Warohingya 700,000 walilazimika kuyaacha makazi yao na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.

Walikimbia huku wakiwindwa na wakiwa na njaa. Wengine waliuawa wakiwa njiani na wengine walizama maji wakijaribu kuvuka na kuingia Bangladesh. Shirika la UN la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) linasema asilima 55 ya wakimbizi hao ni watoto.

Eric Schwartz wa asasi ya kimataifa ya wakimbizi (RefugeeInternational)  anasema haya ni kati ya mauaji makuwa yaliyowahi kutokea duniani. Anaeleza jinsi maelfu kwa maelfu ya wakimbizi walivyolazimishwa kukimbia nchi yao katika muda wa wiki chache.

Kuna ripoti kuhusu wanawake kubakwa, kuuawa na makazi yao kuchomwa moto.

Shirika la kitaifa la haki za binadamu (AmnestyInternational)limetoa ripoti yake ikieleza uhalifu wa kivita na wa haki za binadamu uliofanywa na majeshi ya Myanmar dhidi ya Warohingya wenye imani ya Kiislamu.

Ni pamoja na kuwaua bila ya kuwa na hatia, kuwatesa, kuwafanyisha kazi kama watumwa, kuwanyima chakula, kuwabaka, kuwaua kwa kutumia mabomu ya ardhini na mabomu ya angani.

Imeripotiwa kuwa takriban nyumba 10,000 zimechomwa moto na vijiji vizima vimeteketezwa. Vyanzo vya maji vimefungwa na misaada kutoka nje imezuiliwa

Myanmar imekanusha shutuma hizi kwa kudai kuwa Warohingya nao wamekuwa wakiwashambulia wanajeshi wakiongozwa na kile kinachoitwa jeshi la ukombozi wa Warohingya (Arakan Rohingya Salvation Army).

Hata hivyo wachunguzi wanasema hii haihalalishi kuwashambulia Warohingya wote na kuwafurusha kutoka makwao.

Ubaguzi na udhalilishaji wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar si jambo geni bali limekuwepo kwa muda mrefu. Ingawa wamekuwa wakiishi nchini humo kwa karne nyingi lakini wamekuwa wanahesabiwa kama wahamiaji haramu waliohama kutoka Bangladesh wakati wa utawala wa kikoloni wa Uingereza.

Mwaka 1982 ubaguzi huu ulirasimishwa wakati ilipopitishwa sheria ya kuwanyima Warohingya uraia wa Myanmar. Maana yake wanakosa haki za kiraia kama elimu, matibabu na uhuru wa kwenda watakako.

Ukweli ni kuwa wananchi hawa wanatokana na kabila la Arakan waliokuwa na mfalme wao katika karne ya nane. Ndipo walipoupokea Uislamu kutoka kwa Waarabu waliokuwa wakifanya nao biashara. Idadi yao ikaongezeka na kufikia milioni 1.2 wakiwa wanaishi katika jimbo la Rakhine.

 Mwaka 1784 mfalme wa Burma akashambulia na kuiteka Arakan. Wengi wa wakazi wa Arakan wakakimbilia Bengal (leo Bangladesh). Hali ilipotulia wakarudi Burma. Hata hivyo ubaguzi ukaendelea hadi leo.

Ikumbukwe kuwa India, Bangladesh na Myanmar zimewahi kutawaliwa kwa pamoja na wakoloni wa Kiingereza.

Myanmar ilikuwa na utawala wa kijeshi. Mwaka 2015 uchaguzi ulifanyika na chama cha  National League for Democracy kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kikashinda. Akafunguliwa kutoka kifungoni na kukabidhiwa utawala wa kiraia. Marekani na nchi za magharibi zikamkumbatia Suu Kyi bila ya kujali mauaji ya halaiki yaliyokuwa yakiendelea.

 Suu Kyi aliyekuwa amefungwa kwa miaka mingi akatunukiwa zawadi ya amani ya Nobel na Canada ikamtunuku uraia wa nchi hiyo. Yote haya bila kujali kuwa anafumbia macho mauaji ya halaiki  katika nchi anayoiongoza. Watu wachache walipaaza sauti.

Mojawapo ni Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini ambaye amemlaumu Suu Kyi kwa kufumbia macho mauaji yanayoendelea chini ya uangalizi wake. Tutu akasikitika kuwa nchi nyingi zimekaa kimya badala ya kukemea. Akaongeza kuwa “unapokaa kimya maana yake ni kuwa unaunga mkono”.

Tutu ametuzwa medali ya Nobel sawa na Suu Kyi.

Mtu mwengine ni Papa Francis ambaye amejitokeza na kuwaunga mkono Warohingya. Aliwaombea na kusema “Hawa ni ndugu zetu, ni waungwana na watu wazuri wanaopenda amani”.

Badala ya kuungana na watu kama Tutu na Papa Francis nchi nyingi duniani zimenyamza kimya. Zingine zimekuwa hata zikiusaidia utawala wa Myanmar.

 Kwa mfano Rais Obama wa Marekani ameondoa vikwazo dhidi ya Myanmar kwa sababu eti serikali ya Suu Kyi sasa imechaguliwa kidemokrasia.

Wanaharakati walikumbusha kuwa kuna mauaji yanayoendelea nchini humo lakini Obama hakuwasikiliza wala hakujali ripoti kuhusu mauaji hayo.

Na serikali ya Uingereza nayo ikatenga dola kama 400,000  kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi nchini Myanmar. Waziri wa majeshi wa Uingereza, Michael Fallon aliahidi kutoa mafunzo ya kijeshi kwa Myanmar licha ya mauaji yanayoendeshwa na wanajeshi.

Inasemekana Uingereza imeiuzia Myanmar silaha zenye thamani zaidi ya pauni nusu milioni katika miaka mitatu iliyopita. Kwa kufanya hivyo Uingereza imekwenda kinyume na vikwazo vya kijeshi vilivyowekwa na EU dhidi ya Myanmar tangu 1996.

Misaada ikaingia pia kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Ujerumani, Austria na Israel. Msaada wa Israel kwa majeshi ya Myanmar haushangazi kwa vile hata na wao wamekuwa wakiendesha mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina tangu mwaka 1948 (Nakba).

Wawekezaji nao wakamiminika. Mabilioni ya dola yamewekezwa nchini Myanmar. Mwaka 2018 peke yake zimepangwa dola bilioni sita.

 Wawekezaji wengi wanatoka Uingereza. Wakati alipokuwa waziri wake wa mambo ya nje, Bw Boris Johnson alimsifu Suu Kyi kwa uongozi wake “uliotukuka” na kusema Uingereza unamuunga mkono mia kwa mia. Alipoulizwa kuhusu mauaji Johnson alidai eti “Warohingya si peke yao wanaoteseka”.

Mnamo Novemba 2016  Jenerali Min Aung Hlaing, kamanda mkuu anayehusika na mauaji ya Myanmar alikutana na mwenyekiti wa baraza la kijeshi la Ulaya  ili kujadili jinsi EU itakavyotoa mafunzo kwa majeshi ya Myanmar.

Tena mnamo Aprili mwaka huu jenerali huyo alitembelea Ujerumani na Austria ambako alikutana na kampuni za silaha, akakutana na makamanda wa huko. Austria ikaahidi kumpatia mafunzo kwa askari wake.

Na mnamo Juni mwaka huu aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bw Rex Tillerson (kabla ya kufukuzwa na rais Trump) aliiondoa Myanmar kutoka orodha za nchi zilizowekewa vikwazo kwa kutumia watoto kama wanajeshi.  Maana yake Marekani sasa iko huru kuuza silaha kwa Myanmar.

 Israel imekuwa ikitoa misaada ya kijeshi kwa Myanmar hata wakati ulimwengu ulipoiwekea vikwazo. Waziri wa majeshi wa Israel, Avigdor Lieberman alisisitiza kuwa nchi yake itaendelea kutuma silaha kwa majeshi ya Myanmar.

Hakujali hata alipoambiwa kuwa silaha hizo zinatumika siyo tu dhidi ya Warohingya katika Rakhine bali pia dhidi ya Wakristo walio sehemu za kaskazini.

Ndio maana mnamo Agosti 2016 kampuni ya Isral iitwayoTar Ideal Conceptilitangaza shehena ya bunduki aina ya Corner Shot iliyopelekwa kwa majeshi ya Myanmar.

 Sababu kubwa kwa magharibi “kuisaidia” Myanmar ni kuwa nchi hiyo ina akiba kubwa ya mafuta. Wakati wa vikwazo mafuta haya yalikuwa hayajachimbwa.

Sasa wawekezaji wamo mbioni. Kampuni za mafuta kama Shell, ENI, Total na Chevron zinamezea mate mafuta ya Myanmar. Wameamua kuipiga kikumbo China na kuchukua nafasi yake. 

Sasa tunaona bunge la Canada likipitisha azimio dhidi ya Myanmar na kuitaka nchi hiyo ifikishwe katika mahakama ya ICC. Habari hiyo haikupewa uzito wa kutosha na wala hakuna nchi iliyoungana na Canada.

Hata hivyo habari za mwisho zinaeleza kuwa bunge la Canada sasa limepitisha bila kupingwa azimio la kumvua Suu Kyi uraia wa Canada. Na kuna wengi wanaodai kuwa anyang’anywe pia medali ya Nobel ili kutunza heshima ya tuzo hiyo.

Tayari mnamo Septemba mwaka huu mwendesha mashtaka wa ICC Bi Fatou Bensouda ametangaza kuwa atachunguza shutuma za mauaji ya halaiki nchini Myanmar. Hii ni kufuatia uchunguzi wa UN uliodhihirisha mauaji hayo.

0713-562181

nizar1941@gmail.com

MAONI YAKO