NA AMEIR KHALID

MPIRA wa miguu ni mchezo uliochukua nafasi kubwa duniani kote  hivi sasa kulinganisha na michezo mingine, ingawaje pengine kila nchi ina mchezo wake uliopewa umuhimu.

Mfano nchi ya  Marekani mchezo unaopendwa zaidi ni mpira wa kikapu, Brazil Soka Japan Baseball, lakini kwa hapa kwetu unaweza kusema mchezo ambao unapendwa ni soka, licha  ya kuwepo na michezo mingine.

Lakini katika ulimwengu wa leo unapozungumza michezo, basi      lazima uambatanishe na vyombo vya habari kwani ni watoto pacha wanaostahiki kukuwa na kulelewa pamoja.

Katika kuliona jambo hili linafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana hivi sasa nchi ambazo zinaona umuhimu mkubwa wa waandishi wa habari, wamekuwa na ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha michezo inatangazwa vyema ndani na nje ya nchi yao.

Lakini suala hili kwa hapa Zanzibar linaonekana kuwa ni gumu na linahitaji kazi ya ziada, ili pawepo na maelewano na ushirikiano mzuri baina ya vyombo vya habari na vyama vya michezo kwa kuona michezo inatangazwa kwa faida ya nchi.

Nasema hivi kwa  sababu msimu uliopita hapakuwa na maelewano mazuri sana baina ya waandishi wa habari na viongozi wa ZFA jambo lililosababisha hali ya  sintofahamu.

Wapo ambao wanaweza kulishangaa jambo hili, lakini ushahidi wa Jambo hili upo wa kutosha kabisa, kuwa hakuna maelewano mazuri kati ya waandishi hao na baadhi ya viongozi wa ZFA, hali ambayo kama ilisabaisha baadhi ya waandishi kutaka kugoma kaundika masuala ya ZFA ikiwemo ligi kuu.

Hili si jambo la kupuuzwa hata kidogo kwani, ni wazi kuwa maendeleo ya michezo nchini wanahitaji ushawishi mkubwa kwa kutangazwa katika vyombo vya habari, kama vile leo nchi ya Uingereza ilivyofanikiwa kutangaza soka lao na kuonekana  bora duniani kote.

Katika hili tatizo kubwa ambalo lilitajwa, ni kutokuwepo kwa maelewano mazuri kati ya viongozi hao ni pale waandishi wa habari, wanapodai kuwa wamechoka kutolewa maneno ya kashfa na viongozi hao, huku wakionekana taaluma yao haina thamani licha ya kazi kubwa wanayoifanya ya kutangaza taarifa zao.

Waandishi hawa wamekwenda mbali zaidi kwa kusema viongozi hao wamekuwa wakiwaambia maneno yasiyo ya kiungwana, ambayo yamekuwa yakiwakera na kudhalilisha taaluma yao, jambo ambalo wamechoka nalo kwani  ni muda mrefu sasa wanafanya hivyo licha ya wao kuwavumilia sana.

Walisema kuwa viongozi hao waliwahi kutoa kauli ya kuwa Zanzibar hakuna waandishi, na wao wanawathamini zaidi waandishi kutoka Tanzania bara.

Kutokana na hali hiyo waandishi hao walitaka kuitisha mgomo huo, lakini kwa busara za baadhi yao wakakubaliana kupiga moyo konde na kuendelea kuandika habari zote, ili kuwapa haki yao wananchi ya upata habari.

Ni  ukweli wazi kuwa kuwa kama waandishi hao wangefanya jambo hilo bila ya shaka madhara makubwa yangepatikana, licha ya kuwa baadhi ya watu wahakulipa umuhimu mkubwa na kuona ni jambo la kawaida tu kwao.

Miongoni mwa athari ambazo zingejitokeza kwa ni kuendelea kukosa wafadhili, kwani duniani kote ili mfanyabiashara na mfadhili aweze kudhamini basi anahitaji msukumo mkubwa kutoka kwa vyombo vya habari, kwani hakuna mfadhili anayetoa fedha yake halafu asitangazwe.

Wakati nikilisema hili wapo baadhi yao wanaweza kuhoji kwani waandishi wasipoandika kutakuwa na hasara gani, lakini uhakika ni kuwa kuna athari kubwa sana kama waandishi hao wangesusa kutoa taarifa za ZFA, kwani vyombo vya habari ni muhimili muhimu sana na kwa asiyefahamu thamani yake anaweza kubeza.

Kwa hili niiombe sana ZFA kukaa pomoja na wandishi wa habari mapema kabla ya kuanza kwa ligi kuu, ili kujua nini hasa tatizo lao na kulitafutia ufumbuzi mapema kwa maslahi ya pande zote mbili.

Narudia kusema tena jambo hili kama litaachiwa liendelee na waandishi wakatekeleza nia yao, kwa hakika itakuwa tunaliweka wakati mgumu soka la Zanzibar.

 0774423007

binkhalidson@gmail.com

MAONI YAKO