MATAIFA na jumuiya zenye nguvu za kiuchumi duniani zimeanza kuingia kwenye vita vipya, ambapo vita hivyo havijaeleweka nini itakuwa hatima ya uchumi wa ulimwengu wetu.

Sizungumzii vita vinavyohusisha majeshi yaliyobeba silaha nzito za maangamizi, mizinga, vifaru vya kuboa ngome za maadui, sizungumzii wanajeshi waliomo kwenye nyambizi au walioko angani wakiranda na makombora kwenye ndege za kivita.

Vita vilivyoanzishwa ni vya kibiashara, ambapo muanzilishi mkuu wa vita hivi hasa ni rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye anakabiliana na China kwa upande mwengine.

Kwa sasa Marekani ndio taifa nambari moja duniani lenye nguvu kubwa za kiuchumi, ikifuatiwa na China iliyoko nafasi ya pili ambapo wababe hao wameanza kuingia kwenye vita vikubwa vya kibiashara.

Kwa hakika vita hivi vilivyoasisiwa na Donald Trump, haviihusishi China pekee lakini ndio mlengwa mkuu, pia inazihusisha nchi za Canada na Mexico na ambazo nchi jirani na Marekani, pia jumuiya kubwa ulimwenguni ya Umoja wa Ulaya nayo imetangaziwa vita vya kibiashara ya Trump.

Pamoja na wengine kuhusishwa lakini mlengwa mkuu hasa ni China na msingi wa vita hivi kwa rais Trump wa Marekani kuzipandishia kodi bidhaa zinazotoka China na biadhaa za chuma cha pua na aluminiamu kutoka Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico una lenga kupunguza urari wa biashara kwa bidhaa za nje.

MAONI YAKO