NA AMEIR KHALID

KIPINDI cha hivi karibuni tumeshuhudia viongozi wakuu wa chama cha soka Zanzibar ZFA, wakijiuzulu nafasi zao, baada ya sakata zima la timu ya taifa ya vijana U-17 kutolewa katika mashindano ya Cecafa.

Viongozi hao ni rais wa ZFA Ravia Idarous Faina na Makamu wake wawili Ali Mohamed Pemba na Mzee Zamu wa Unguja, hatua ambayo baadhi ya watu wanauliza kwa nini kamati tendaji nayo isichukuwe maamuzi hayo.

Lakini kujiuzulu kwa viongozi hao pia ni hatua moja muhimu ya kupata viongozi wapya, ambao wataongoza chama hicho kwa mujibu wa katiba ya chama ambayo inatumika hivi sasa.

Walio wengi hivi sasa wanahamu kubwa sana ya kuona unaitishwa uchaguzi mwengine kuziba nafasi hizo tupo za juu, ili kuendeleza mpira wa Zanzibar ambao tayari hivi sasa umeelekea kaburini.

Kutokana hamu kubwa ya wadau na wananchi wa Zanzibar ambao wana lengo la kutaka kugombea nafasi hizo, tayari baadhi ya watu wameanza kutangaza nia ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya hizo.

Lakini wakati hatua ya baadhi ya wananchi hao wakiweka nia hiyo kuna mambo mawili makubwa ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka sana ili kuweka mambo sawa.

Jambo la kwanza ambalo mimi naona linahitaji maelezo ya haraka lakini hadi sasa sijaona kufanyiwa kazi na kunipa mashaka kidogo, ni ukimya wa kamati ya uchaguzi ya ZFA ambayo hadi sasa bado haijasema kitu huku wananchi wakiwa hawaelewi nini kinaendelea.

Niseme wazi unapotaja suala la mpira wa miguu hivi sasa ni jambo ambalo linawawahusu mamia ya Wazanzibari ambayo kwa miaka mingi wamekuw wakiumizwa sana na maendelea finyu ya mpira wa migtuu hapa Zanzibar.

Sasa kwanini leo viongozi ambao walikuwa wakiongoza soka wameondoka madarakani lakini vyombo husika vimekaa kimya na wala hukana taarifa zozote ambazo zinatolewa, iwe kufanyika uchaguzi au jambo gani linaendelea, hili si sawa na niwaombe sana kamati hii kujaribu kusoma alama za nyakati.

Jambo la pili ambalo kwa haraka sana nahisi kama halitofanyiwa kazi haraka kabla ya kuelekea katika huyo uchaguzi ambao hadi sasa upo kwenye kiza kinene, ni suala zima la kuwa na katiba mpya ambayo itakidhi haja ya soka la kisasa.

Miongoni mwa mambo ambayo yanawakera na kuwaudhu mno wadau wa soka Zanzibar ni katiba mbovu, ambayo inaendelea kutumika kwenye kuendedsha soka la Zanzibar, kiasi ambacho limepelekea kufa na kuzikwa kabisa mchezo huo.

Katiba ya ZFA ya mwaka 2010 kwa kiasi kikubwa ndio hasa adui mkubwa soka letu, ambayo hivi sasa watu wengi hawapendi hata kuisikia seuze kutumika kuongoza soka, ambayo inadaiwa kuendekeza zaidi Upemba na Uunguja katika kuongoza soka ndani ya nchi moja jambo linaloleta mgawanyiko mkubwa.

Ni ukweli uliowazi na wala tusijidanganye kama katiba hii ya sasa haitafanyiwa mabadiliko makubwa, basi hakuna mageuzi yoyote yatakayofanyika katika soka letu hata aje rais wa FIFA awe ndiye rais wa ZFA.

Basi kwa heshima na unyenyekevu mkubwa kabisa niziombe mamlaka husika juu ya suala la marekebisho ya katiba ya ZFA, basi wasilichukulie kwa wepesi jambo hili, au kama vijana wa leo wanaposema ‘wasilichulie poa’, kwa uzingatia kuwa ni msingi wa maendeleo ya soka letu.

Pia wakumbuke kuwa kwa muda mrefu sasa Wazanzibari wameumizwa na katiba hii mbovu ambayo inaongoza soka letu na ilifanywa kwa maslahi ya watu Fulani, hivyo basi umefika muda sasa yale maslahi ya watu fulani yageuzwe  kuwa ni maslahi ya Wazanzibari wote.

Nimeamua kulisema hili ili kuwasilisha kilio ch wananchi wengi ambao pengine sauti zao ni ndogo na hawajui wapi wanaweza kupeleka zikasikika na kufanyiwa kazi kwa haraka kwa maslahi ya wote.

Hili likitiliwa maanani na kuonekana ni la nchi basi soka la Zanzibar linaweza kufufuka kurudi kwenye hadhi yake kama zamani, endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake.

0774423007

binkhalidson@gmail.com

MAONI YAKO