1.MCHEZAJI wa timu ya mpira wa Kikapu kanda ya Unguja Salum Bakari (kulia) akimtoka mchezaji wa mkoa wa Dar es Salaam, wakati timu hizo zilipokutana kwenye robo fainali ya mashindano ya Umisseta.Unguja ililala kwa vikapu 75-42.(PICHA NA AMEIR KHALID)

NA AMEIR KHALID, MWANZA

ZANZIBAR imeanza kupata vikombe vya mashindano ya Umisseta baada ya jana timu ya mpira wa Meza (Table tennis), kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa wanaume na wanawake.

Katika mchezo huo kwa upande wa wanaume mchezaji Sultani Suleiman aliibuka na ushindi baada ya kushinda kwa seti 2-0 dhidi ya Dar es Salaam, na Mwanajuma Bakari alishinda seti 2-0 mkoa wa Mwanza.

Mbali na timu hizo kutwaa ubingwa, timu ya mpira wa mikono imetinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 20-17 dhidi ya mkoa wa Tabora mchezo ambao ulikuwa mgumu, kwani licha ya kufungwa Tabora walionesha kiwango kizuri na kutoa upinzani kwa Unguja.

Mchezo mwengine ambao kanda ya Unguja imetinga hatua ya fainali ni riadha mita 200 baada ya mkimbiaji Nassra Abdalla kuibuka mshindi wa kwanza kwa wanawake, na kwa upande wa wanaume mkimbiaji Mohamed Rashid ameingia fainali baada ya kupata nafasi ya kwanza mita 200, huku Omar Rashid naye akiibuka mshindi wa pili katika mbio hizo na kutinga fainali.

Katika mbio za mita 100 x 4 (Relay) upande wa wanawake Unguja imeingia fainali baada ya kupata nafasi ya kwanza kwenye hatua ya nusu, wakati wanaume wameingia hatua ya fainali baada ya kupata nafasi ya pili,pia Unguja itacheza hatua ya fainali leo katika mbio za mita 200 wanaume na wanawake pamoja na kuruka juu.

Hata hivyo timu ya mpira wa kikapu imetolewa katika hatua robo fainali baada ya kupokea kipigo cha vikapu 75-42 dhidi ya Dar es Salaam, hivyo kuzima ndoto za kanda ya Unguja kufika hatua ya nusu fainali.

MAONI YAKO