Waziri wa wizara hiyo, Dk. Khalid Salum Mohamed

HAFSA GOLO NA NASRA MANZI

WIZARA ya Fedha na Mipango, imekusudia kutekeleza vipaumbele vinane, programu saba, miradi minane na kukusanya shilingi trilioni 1.28 katika mwaka wa fedha 2018/19.

Waziri wa wizara hiyo, Dk. Khalid Salum Mohamed, alieleza hayo jana wakati akisoma hutuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka ujao wa fedha katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.

Alisema miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji mapato ya ndani, kuandaa dira mpya ya maendeleo ya taifa, kufanya sensa ya kilimo Zanzibar na kufanya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya.

Kuhusu progrmu zitakazosimamiwa katika mwaka ujao alisema ni programu ya usimamizi wa bajeti na fedha za umma ambayo inatarajiwa kutumia shilingi bilioni 57.86, programu ya usimamizi na uwekaji wa mali za umma nayo inakaridiwa kutumia shilingi bilioni 19.92 pamoja na programu ndogo mbili ikiwemo ya usimamizi wa mitaji ya umma, ununuzi na uhakiki wa mali za serikali.

Kuhusu utekelezaji wa miradi, alisema ni pamoja na utekelezaji wa mradi wa kuimarisha huduma za jamii, kuimarisha upatikanaji wa rasilimali fedha na kuimarisha utawala bora.

Alitaja muelekeo wa bajeti katika mwaka wa fedha 2018/19 na baadhi ya taasisi na mashirika yanayotarajiwa kukusanya fedha kwa ajili ya maendeleo, uchumi na serikali kwa ujumla.

Alisema Bodi ya Mapato Zanzibar imepangiwa kukusanya mapato ya shilingi bilioni 485.33, Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi (ZIPA) shilingi bilioni 3.75, mfuko wa barabara shilingi 15.63 bilioni, shirika la bima shilingi 28.5 bilioni, Benki ya Watu wa Zanzibar shilingi 70.5 bilioni na ZSSF shilingi 116.95 bilioni.

MAONI YAKO