WAZIRI wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Maher Al Barwany muendesha Pikipiki kutoka Oman katika ukumbi wa Wizara ya Habari uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar alipofanya ziara ya kitalii Visiwani Zanzibar, katikati ni Balozi Mdogo wa Oman Zanzibar Dkt. Ahmed Hamoud Al Habsy.

NA SALUM VUAI, WHUMK

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, amesema ziara inayofanywa na Maher Al Barwani, raia wa Oman kulizunguka bara la Afrika kwa pikipiki ni fursa nzuri ya kutangaza utalii na kupeleka ujumbe wa amani duniani.

Maher (37), yuko Zanzibar takribani wiki moja sasa tangu aingie Afrika, katika mfululizo wa ziara zake alizozianza Julai 22, 2017 kutokea Muscat akipitia Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia.

Akizungumza ofisini kwake katika hafla ya kumkaribisha Maher ambae ana asili ya Zanzibar, alisema kitendo hicho ni cha kishujaa kwani si nchi zote zina amani kama ilivyo Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Alisema Zanzibar inajivunia kumuona kijana kama huyo ambaye msingi wa kizazi chake umetokea hapa, kupata wazo la kuitembea dunia kwa njia ya pikipiki yenye manufaa badala ya kukitumia chombo hicho kwa michezo ya hatari.

Alisema uamuzi wa Maher kufika Zanzibar baada ya kuizunguka Tanzania Bara, ni sahihi kwani ndiko iliko historia ya kuvutia zaidi kuhusu Oman kuliko nchi nyengine yoyote Afrika.

Alieleza kuwa, tangu Julai 22, 2017 alipoanza nchini Oman, tayari barani Afrika ameshafika Sudan, Ethiopia, Kenya, Uganda, Rwanda Burundi na Tanzania Bara kabla hajapanda meli kuja Zanzibar.

Hafla ya kumkaribisha, ilihudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale ikiwemo Kamisheni  ya Utalii, pamoja na Balozi mdogo wa Oman Zanzibar, Dk. Ahmed Hamood Al Habsy.

MAONI YAKO