NA MWANDISHI WETU

WAISLAMU wakiwa wanaelekea kumaliza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na tayari kwa maandalizi ya Sikuu ya Idd el – Fitri, kuna umuhimu wa kuangazia umuhimu wa utoaji wa Zakaatul-Fitri kwao.

Ni nini hiyo Zakaatul – Fitri?

Zakaatul-fitri ni kile chakula kinachotumika zaidi na watu wa jamii husika na kutolewa na mfungaji mwishoni mwa mwezi wa Ramadhani na kuwapa wanaostahili kupewa zaka kabla ya swala ya Idd el-Fitri kuswaliwa.

Nini hukumu yake?

Zakaatul-Fitri ni fardhi mbele ya kundi kubwa la wanazuoni. Ufaradhi huu unatokana na hadithi iliyopokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi – yeye amesema:

“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-Amefaradhisha Zakaatul-Fitri ya Ramadhani. Pishi la tende au pishi ya shayiri, kwa mtumwa na muungwana, mwanamume na mwanamke, mtoto na mkubwa katika Waislamu. Na ameamrisha itolewe kabla ya watu kutoka kwenda kuswali (yaani swala ya Eid).” Bukhaariy & Muslim.

Mtume Muhammad (S.A.W), ameifaradhisha Zakaatul-Fitri na kuamrisha itolewe katika mwaka ule ule uliofaradhishwa swaumu ya Ramadhani. Yaani katika mwezi wa Shaaban, mwaka wa pili wa Hijrah.

Nini falsafa yake?

Zakaatul-Fitri imefaradhishwa kwa hekima nyingi, miongoni mwake ni kuwasaidia wenye shida katika siku hii ya sikukuu ili furaha ienee kwa watu wote.

MAONI YAKO