NA MWINYIMVUA NZUKWI
SERIKALI ya mkoa wa Mjini Magharibi, imeeleza kuwa inaangalia uwezekano wa kuonesha mechi ya kwanza ya ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Dunia baadae wiki hii kama ilivyokuwa katika fainali za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi uliopita.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,Ayoub Mohammed Mahmoud, alieleza hayo katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga na kuongeza kuwa hatua hiyo imelenga kutoa fursa kwa mashabiki wa soka wa mkoa huo kukusanyika pamoja na kushuhudia uzinduzi wa tamasha hilo kubwa kwa mchezo wa soka ulimwenguni.

Alisema, ofisi yake inawasiliana na wadau wengine walioshirikiana kuonesha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ili kuona uwezekano wa kuongeza mchezo huo baada ya hapo awali wadau hao kuahidi kuonesha michezo ya kuanzia nusu fainali ya mashindano hayo yatakayoanza siku ya Alkhamis nchini Urusi.

“Siku ya ufunguzi tutakuwa bado tupo katika mfungo kama mwezi hautoonekana mapema na kufanya ibada ziendelee hivyo haitokuwa vyema wakati ibada zikiendelea na sisi tukawa katika masuala ya burdani”.

“Lakini tunaangalia mapishano ya muda kama yatakuwa yanapishana sana tutaonesha mechi hiyo pamoja na zile tulizoahidi awali”,alisema.

Hivyo, aliwaomba wananchi wa mkoa huo kutumia mashindano hayo kuimarisha upendo na uhusiano mwema miongoni mwao kwa kuepuka mifarakano ili kuleta umoja jambo ambalo ni miongoni mwa falsafa za mchezo wa soka.

MAONI YAKO