HAFSA GOLO NA HANIFA RAMADHANI

WIZARA ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo imewashauri wapiga kura katika klabu za michezo ya mpira wa miguu, kuhakikisha wanachagua viongozi wa ZFA wenye uwezo wa kuongoza soka na si kuangalia maslahi yao.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo Lulu Msham,alieleza hayo jana katika ukumbi wa baraza la Wawakilishi wakati akijibu suala lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la Rahaleo Nassor Jazira, kuhusiana na migogoro ndani ya chama hicho jambo ambalo linachangia kudumaza soka la Zanzibar.

Alisema wajumbe hao wanapaswa kuchagua viongozi makini na wenye ujuzi wa kuendesha masuala ya mchezo wa mpira wa miguu nchini, ili kuondosha mivutano isiyo na tija.

Aidha alisema ni vyema viongozi wa ZFA wakajitathmini juu ya utendaji wao ambao umekuwa ukilalamikiwa na baadhi ya wapenzi wa soko nchini.

“Kila miaka minne hufanyika uchaguzi wa kuwachagua viongozi wa ZFA, hivyo wapigaji kura tumieni fursa hiyo kuchagua viongozi wenye uwezo” alisema.

Kuhusu suala la ujenzi wa viwanja vya michezo katika wilaya alisema, katika kipindi cha mwaka 2016/17, ilianza ujenzi wa kiwanja cha Kitogani na kwa hatua ya awali umekamilika na tayari unaendelea kutumika.

MAONI YAKO