NA ASYA HASSAN

SERIKALI ya Wilaya ya Kati imeitaka jamii kuisaidia serikali kuwafichua wale wote waliosababisha kifo cha mtoto Elizabeth Ndauli Ikobeko mwenye umri wa miaka minane mkaazi wa Bambi, wilaya ya Kati Unguja.

Mkuu wa wilaya hiyo Mashavu Sukwa alisema hayo baada ya kufika eneo la Bambi kwa Matthias ambapo ndipo ilipotumwa maiti ya mtoto huyo kwenye kichaka.

Alisema, mtoto huyo aliondoka nyumbani kwao Mei 14 asubuhi akielekea skuli na hakurudi tena na badala yake alikutwa kichakani akiwa ameshafariki.

Alifahamisha kuwa maiti ya mtoto huyo ilikutwa Mei 15 baada ya mtu mmoja ambae jina lake halikupatikana na gazeti hili kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kukata majani ya ng’ombe ndipo alipokuta maiti ya mtoto huyo katika kichaka hicho.

Mkuu huyo alisema ukatili huo hauwezi kuvumilika hivyo ni vyema jamii kutoa mashirikiano ya kuwafichua wale wote waliohusika na tukio hilo kwa namna moja au nyengine ili kuweza kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Kifo cha mtoto huyu kimetokea katika mazingira ya kutatanisha kutokana na maiti yake kukutwa ikiwa imetupwa kichakani,ambapo inawezekana kuna watu wamefanyiwa hujuma mtoto huyo na halafu kumtupa kichakani,”alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja Makarani Khamis Ahmed alisibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba hivi sasa bado mapema kutuo sababu za kifo hicho ila jeshi la polisi linaendelea na upelelezi wa tukio hilo.

MAONI YAKO