NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

KATIBU mkuu wizara ya Mambo ya Kale wa Serikali ya Kifalme ya Oman, Salum Mohamed Al-Mahrooq amesema uwepo wa jumla la Bait al Ajaib na Mjimkongwe, ni kielelezo na utambulisho wa Zanzibar kihistoria, kiutamaduni na kimataifa.

Al-Mahrooq alieleza hayo akiwa ameambatana na Balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar, Ahmed bin Humoud Al Habsy, wakati kwneye mazungumzo ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Alisema jengo hilo maarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani, limejengwa tangu karne ya 17 na kwamba linastahiki kufanyiwa matengenezo makubwa ili kulirejeshea hadhi yake.

Katibu huyo alisema serikali ya Oman, imejitolea kugharamia matengenezo ja jengo hilo, ambapo limekuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii katika Mjimkongwe.

Al-Mahrooq alisema hatua ya serikali ya Oman gharama za matengenezo ya jengo hilo, imekuja kutokana na historia kubwa ya uhusiano wa karibu uliopo kati ya Zanzibar na Oman kwa karne kadhaa zilizopita.

Alisema historia ya pande hizo mbili zenye udugu wa damu hasa katika masuala ya utamaduni, utaendelea kuwepo na kuimarishwa kwa faida ya vizazi vya sasa na vile vya baadae.

Alimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kwamba ujio wa ujumbe wake kufanya ziara visiwani Zanzibar utaanzisha uratibu wa ushirikiano wa mambo kadhaa yatanayoweza kusaidia kuimarisha ushirikiano baina ya Oman na Zanzibar.

MAONI YAKO