LONDON, England

WINGA, Mohamed Salah, amevunja rekodi ya ufungaji mabao katika Ligi Kuu ya England baada ya kuwafungia Liverpool magoli 38 ya michuano yote msimu huu.

Hilo ni moja tu kati ya matukio muhimu yaliyotokea siku ya mwisho ya msimu huu wa 2017/18 wa Ligi Kuu ya England.

Magoli ya Salah yaliwasaidia Liverpool kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Goli la Salah la 32 ligini msimu huu, lilimuwezesha kuwapita Alan Shearer, Cristiano Ronaldo na Luis Suarez.

Dejan Lovren alifunga kwa kichwa, Dominic Solanke akafungia Liverpool bao lake la kwanza naye Andrew Robertson akafunga jengine na kukamilisha ushindi wa 4-0 wa klabu hiyo ya Anfield dhidi ya Brighton.

Klabu hiyo ilikuwa inahitaji pointi moja pekee kuwapita Chelsea na kujikatia tiketi ya kucheza ligi hiyo msimu ujao.

Chelsea ambao walipokea kichapo cha kushangaza na Newcastle sasa watacheza Ligi ya Europa baada ya kumaliza nafasi ya tano.

Hata hivyo, ushindi wa Liverpool haukutosha kuwafikisha nafasi ya tatu kwenye msimamo ambayo ilitwaliwa na Tottenham waliopata ushindi wa 5-4 dhidi ya Leicester kwenye mechi ambayo huenda ikawa yao ya mwisho kuchezea Wembley kama uwanja wao wa nyumbani kabla ya kuhamia tena White Hart Lane.

Vijana hao wa Mauricio Pochettino walijikuta nyuma mara tatu, lakini, Erik Lamela na Harry Kane walifunga mabao mawili kila mmoja, Kane akifikisha magoli 30 ligini naye Christian Fuchs akajifunga na kuwapa ushindi.

Mwenzake Kane katika timu ya taifa ya England, Jamie Vardy, alifunga mabao mawili pia lakini kwa upande wa Leicester.

Iwapo Liverpool wangelishindwa na Brighton, bado wasingelikosa nafasi ya kumaliza katika nafasi ya nne baada ya Chelsea kulazwa 3-0 ugenini Newcastle.

Ayoze Perez alifunga mabao mawili baada ya Dwight Gayle kufungua ukurasa wa mabao na kuhakikisha Newcastle wakiwa mikononi mwa Rafael Benitez wakimaliza nafasi ya 10.(BBC Sports).

MAONI YAKO