Ubebaji dawa za kulevya wachafua

NA ABDI SHAMNAH

MKURUGENZI wa Kampuni ya Mabaharia ya Danous, Mzee Ali, amesema tamaa, kutokinai na kuacha kumtanguliza mbele Mwenyezi Mungu ndio chanzo cha mabaharia wa Tanzania kujiingiza katika matukio ya usafirishaji wa dawa ya kulevya.

Alisema hayo katika mkutano wa mabaharia uliofanyika mwishoni mwa wiki na kuwahusisha wafanyakazi na viongozi wa juu wa kampuni za ubaharia ya Danous iliopo Zanzibar, ikiwa ni hatua ya kupinga usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia mabaharia wa Kampuni hiyo.

Imeelezwa kuwa kabla kampuni hiyo ilikuwa na mabaharia karibu 1,000 wanaosafiri na meli za nje katika nchi mbalimbali Duniani, lakini hivi sasa ni mabaharia 200 pekee waliobaki wakifanyakazi katika meli hizo.

Jumla ya mabaharia wanane wamefungwa katika nchi mbalimbali, baada ya kukamatwa na dawa za kulevya, huku 15 wakidaiwa kujiripuwa kwa kile kinachoelezwa kutafuta maisha, jambo lililioitia aibu Kmapuni ya Danous na Tanzania kwa ujumla.

Alisema Mwenyezi Mungu amewawaumba wanaadamu na kuwapa akili ili watambue mazuri na kuyafuata, lakini jambo la kushangaza mbali na kuisoma dini yao na kupata kazi za kusaidia familia zao, wanakufuru na kuibeza neema waliyoipata.

Akioneshwa kukasirishwa na tabia hiyo, alisema watu wengi wanatafuta nafasi kama hizo ili ziwasaidie na familia zao bila mafanikio, huku wale wanaozipata wanazichezea na kuhatarisha maisha yao kwa kusafirisha dawa za kulevya.

“Usafirishaji wa dawa za kulevya ni hatari na yana madhara makubwa sio tu kwa mabaharia lakini hata kwa mtu binafsi, familia na hata nchi kwani duniani kote hivi sasa yanapigwa vita”, alisema.

Nae, Kapteni Stelios Petronios kutoka Ugiriki, alisema kuna changamoto kubwa inayowakabili mabaharia  hivi sasa, ya kujiingiza katika katika usafirishaji wa dawa za kulevya, jambo linalopigwa vita duniani kote.

Alisema vita ya kupambana na dawa za kulevya ni vigumu, kutokana na wanaofanya biashara hiyo wana mtandao mkubwa na wameenea dunia nzima, hivyo akabainisha jambo muhimu kwa mabaharia ni kutumia njia ya kuheshimu kazi yao na kuzijali familia zao.

MAONI YAKO