NA MWANDISHI WETU

MWAKILISHI wa Jimbo la Chwaka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu amewakabidhi mabalozi wa CCM zaidi ya baiskeli 500 katika jimbo hilo ambalo liko wilaya Kati Mkoa Kusini Unguja.

Akizungumza na wananchi katika kijiji cha Marumbi, Gavu alisema kwamba ugawaji wa baiskeli hizo kwa mabalozi na viongozi wa jumuiya za CCM ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ikiwa pamoja na ahadi yake kwa wanachama wa chama hicho ngazi ya mashina kuwapatia baiskeli.

“Kama mtakumbuka wakati wa kampeni tuliahidi kuwapatia mabalozi wetu wote baiskeli, tumekuja hapa kuwakabidhi baiskeli zenu, CCM siku zote inaahidi na kutenda”, alisema Gavu.

Mwakilishi huyo alisema kwamba kukabidhiwa kwa baiskeli hizo ni hatua ya mwanzo katika kuwarahisishia usafiri ambapo awamu ya pili ni kutolewa kwa piki piki kwa viongozi wote wa ngazi ya wadi na jimbo.

“Ndugu wanachama wenzangu wa CCM, baiskeli tulizogawa ni kwa mabalozi, viongozi wengine kuanzia ngazi ya wadi hadi jimbo tutawapa piki piki… vuteni subira kidogo muda sio mrefu mtapata”, alisema.

Akizungumzia tatizo la maji katika kijiji cha Uroa, Mwakilishi Issa Gavu alisema kwamba tayari tatizo hilo limeshapatiwa ufumbuzi na wakati wowote kuanzia mwezi huu, mafundi wa Mamlaka ya Maji Zanzbar (ZAWA) wataanza kazi ya kulaza mabomba katika kijiji hicho.

Akizungumza katika mkutano huo akiwa mgeni mwalikwa, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki na Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo alisema jimbo la Chwaka ni jimbo la dhahabu kwa Mwakilishi wao namna anavyotekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Nataka nikwambieni watu wa Chwaka, jimbo lenu ni jimbo la dhahabu, Mwakilishi wenu anajituma na anawajibika hasa, kazi anazofanya ni kubwa na za kupigiwa mfano msije mkafanya mzaha mkimpoteza itawachukua miaka mingi kupata mwakilishi kama huyo”, alisema waziri Mahmoud.

Waziri Mahmoud alisema kwamba serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein inaendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi na kwamba Zanzibar inaendelea kushuhudia mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii.

MAONI YAKO