KAMA kuna msaada mkubwa anaoweza kuutoa binaadamu kwa binaadamu mwenziwe, bila shaka ni pale unapojitolea kuokoa maisha yake wakati anapokuwa hajiwezi, mahututi na kwamba atakapokosa msaada huo anaweza kupoteza maisha.

Binaadamu kamwe hawezi kuishi duniani endapo atakuwa na upungufu wa damu, kwani hata ukimpa mali zote ulimwenguni wakati akiwa hana damu hazitakuwa na maana kwa sababu uhai wake uko hatarini.

Ni wazi zawadi ya kipekee ya kumpatia mwanadamu ni pale unapookoa maisha yake kwa kumsaidia damu wakati anapokuwa na haja ya kupatiwa masaada huo ili kuyaondoa maisha yake hatarini.

Mataifa karibu yote duniani yameweka utaratibu wa benki ya damu salama, kwa sababu kikawaida hutokea mambo ya dharura ambayo bila ya kusubiri hata dakika chache binaadamu huhitaji kupatiwa damu ili maisha yake yasipotee.

Katika jamii yetu, wengi tumekuwa wahitaji wakubwa wa damu hasa pale wake zetu wanapojifungua hasa kwa upasuaji au kuwa na wagonjwa wa maradhi mbalimbali wanaohitaji kufanyiwa operesheni.

Huku tukiwa na mahitaji hayo na tukifahamu umuhimu wa damu kwa ajili ya kunusuru maisha ya wapendwa wetu, tatizo kubwa tunaloliona ni kwamba jamii imekuwa na usiri mkubwa katika kujitolea kuchangia damu.

Hebu tujiulize, kama wengi wetu katika jamii wamekuwa wakihitaji damu, lakini wakati huo huo tumekuwa wagumu kuchangia hivi maisha ya wapenda wetu yataokolewa na nani?

Watu wengi wamekuwa wazito kuchangia damu, hafo yao inakuja wakati wa kupima usalama wa damu hiyo, ambapo wanahisi vitu vingi vinaweza kujitokeza hasa maradhi.

Sijui nini kinawatia hofu wakati damu hiyo inapopimwa kabla ya kutolewa ndiyo inakupa fursa ya kujitambua uzima wa afya yako na damu yako kwa ujumla, sasa hili pia ndio liwape uzito?

Wengine hujitia sababu eti damu waliyonayo mwilini mwao haitoshi bila ya hata kwenda kupata uthibitisho wa wataalamu juu ya kiwango chao cha damu walichonacho mwilini. 

Kwa mujibu wa taarifa za benki ya damu salama Zanzibar, kwa mwezi wagonjwa wetu wanaolazwa katika hospitali mbalimbali wanahitaji wastani wa chupa 1,250.

Ukweli ni kwamba chupa hizi sio nyingi hata kidogo na tunaweza tusiwe na tatizo la damu salama endapo jamii itachukuliwa kuwa uchangiaji damu ni wajibu wetu.

Aidha taarifa zinafahamisha kuwa kila kinapofika kipindi cha mwezi mtukufu wa wa Ramadhani, Zanzibar huwa ndio inakumbwa na uhaba mkubwa wa damu na hivyo kulazimika kuomba msaada kutoka Tanzania bara.

Tunafikiri umefika wakati jamii kujitolea kwa hiyari kuchangia damu, kwani matumizi yake ni kuokoa maisha ya wapendwa katika jamii yetu.

Ni vyema tukahamasishana ili jamii iweze kujitolea kuchangia damu salama lakini zaidi tujikite kuwatoa hofu wale wenye dhana zisizo na msingi.

MAONI YAKO