DUNIA inaendelea kukabiliwa na kitisho kikubwa cha dawa za kulevya, ambapo uraibu huo umekuwa ukipoteza nguvu kazi, hali inayodhoofisha uchumi wa mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Imekuwa vigumu kuachana na biashara ya dawa za kulevya kwa sababu wenye kufanya bishara hiyo wanajipatia utajiri mkubwa na wale watumiaji imekuwa vigumu kuacha.

Katika makala haya ningependa kukutajia orodha ya wauza dawa za kulevya walioutikisa ulimwengu na hatimaye kupatikana na hatia kwa kufungwa na wengine kuuawa.

Frank Lucas maarufu kama ‘Superfly’

Unapowazungumzia wauza dawa za kulevya wakubwa ambao wamewahi kuishi katika hii dunia basi hutoweza kuliacha jina la Frank Lucas, ambaye anajulikana kwa jina maarufu la ‘Superfly’.

Frank Lucas ni raia wa Marekani, aliyezaliwa Septemba 9, mwaka 1930 ambapo inakadiriwa kuwa biashara ya dawa za kulevya hasa ‘heroine’ imemuwezesha kupatia utajiri mkubwa unaofikia dola bilioni 52.

Mfanyabiashara huyo wa dawa za kulevya alivuma sana katika miaka ya mwishoni mwa mwaka 1960 na mwanzoni mwa mwaka 1970. Mbinu kubwa alitokuwa akiitumia kusafirisha dawa hizo ni kupitia majeneza ya watu waliouawa na genge lake lilokuwa likimtii.

Mnamo mwaka 1975, ‘Superfly’ alivamiwa nyumbani kwake, ambapo ndani ya   nyumba yake kukakutwa kiasi cha dola 500,000, ambapo kwa wakati huo zilikuwa fedha nyingi sana.

Polisi walimfungulia mashitaka na hivyo mahakama ikamtia hatiani ambapo alipewa kifungo cha miaka 70 jela kutokana na mashitaka kadhaa ya dawa za kulevya yaliyokuwa yakimkabili.

Christopher Coke maarufu kama ‘Dudus’

Jina jengine kubwa ulimwenguni kwenye biashara ya dawa za kulevya ni Christopher Coke aliyekuwa akijulikana kwa jina maarufu kama “Dudus”.

Mfanyabishara huyo mkubwa wa dawa zakulevya, alizaliwa Machi 13 mwaka 1969, katika kitongoji cha Tivoli Gardens kwenye jiji la Kingston, nchini Jamaica.

Christopher Coke ama ‘Dudus’, ni jamaa aliyeonekana mwenye sura ya upole, lakini alikuwa mpiga dili mkubwa kwenye biashara ya dawa za kulevya.

Mjamaika, huyo alikuwa na sifa ya kusaidia watu ambapo baada ya kugundulika kwamba anafanya biashara hiyo, hakutaka hata kutafutwa, bali alijisalimisha mwenyewe polisi mwaka 2010.

‘Dudus’ aliingiza kiasi kikubwa cha fedha, mpaka akamatwa alikuwa ameingiza kiasi cha dola bilioni 30, ambapo kwa sasa tungempigia hesabu kuwa miongoni mwa matajiri 20 wakubwa duniani.

Japokuwa alikuwa na ubaya wake wa kufanya biashara hiyo haramu lakini alikuwa mtu wa watu, kwani alijenga hospitali, kufanya biashara nyingine na kuajiri watu wengi.

Kupitia utajiri wake wa haramu, aliwasaidia masikini na kuwafurahisha kwa kuyaboresha mazingira yao japokuwa upande wa nyuma, aliteketeza vijana kwa kuwauzia biashara hiyo.

Mwezi Mei mwaka 2011, mahakama mjini New York nchini Marekani ilimfunga ‘Dudus’ miaka 23 jela ambapo mbali ya kupatikana na hatia ya kuingiza dawa za kulevya nchini Marekani pia alipatikana na hatia ya kusafirisha silaha.

Griselda Blanco “The Cocaine Godmother”.

Kama ulikuwa unafikiri kuwa majina ya wanaume tu ndiyo yaliyoko kwenye orodha ya juu kwenye biashara ya dawa kulevya duniani, basi umekosea sana, kwani lipo jina la mwanadada mashuhuri sana kwenye biashara hiyo.

Mmoja kati ya mwanadada wa shoka waliotikisa dunia kwenye biashara hiyo ni Griselda Blanco ambaye kwa jina maarufu anajulikana kama likuwa akijulikana kama “The Cocaine Godmother”.

Griselda Blanco alikuwa mtu mhimu sana kwenye uendeshaji wa dili za biashara ya dawa za kulevya, ambapo alizaliwa Februari 15 mwaka 1943 katika mji wa Cartagena nchini Colombia.

Mbali na kujishughulisha na biashara hiyo, alikuwa dada katili mno ambapo kwa kipindi chote alichofanya biashara hiyo inakisiwa aliwaua kwa kuwapiga risasi kiasi cha watu 200 kwa kutumia mikono yake, mbali ya aliotumisha wauawe.

Baada ya kufanya biashara hiyo kwa miaka kadhaa, akakamatwa na kufungwa miaka 20 gerezani, ila cha kushangaza sasa, akiwa hukohuko nyuma ya nondo, michongo yake ya kibiashara ilikuwa ikisonga kama kawaida.

Mwaka 2004 akatolewa gerezani, lakini ilipofika mwaka 2012, akauawa kwa kupigwa risasi na mtu aliyekuwa akiendesha pikipiki huko katika mji wa Medellín nchini Colombia.

Huo ukawa mwisho wa maisha yake na kuzikwa ingawa bado anajulikana kama mfanyabiashara mkubwa wa biashara hiyo haramu.

Rick Ross maarufu kama “Freeway”

Rick Ross tunayemzungumza hapa sio yule mwanamuziki wa kimarekani mwenye mwili mkubwa. Hapa tunamzungumzia Rick Ross mwneye mwili wa kati na tajiri mkubwa wa dawa za kulevya.

Rick Ross mwanamuzi, unayemtambua amechukua jina kutoka kwa Rick Ross mfanyabishara wa dawa za kulevya aliyezaliwa Januari 26 mwaka 1960, huko Texas, nchini Marekani.

“Freeway” ni mtashati aliyependa kutabasamu, lakini nyuma ya tabasamu lake, jamaa alikuwa mbaya kwenye biashara ya dawa za kulevya, kwani kwa wiki alikuwa akiuza kiasi cha kilo 455 na kuingiza kiasi cha dola milioni 3.

Alianza kufanya biashara hiyo miaka ya 1980, ambapo alianza kama msambazaji wa dawa za kulevya baadaye akajidhtiti na kuwa na biashara yake mwenyewe.

Arturo Beltrán Leyva maarufu kama “Boss of Bosses”

Arturo Beltrán Leyva kama walivyo wafanyabishara wengine alikuwa akiongoza kundi linalojishughulisha na biashara hiyo liitwalo Beltran Leyva Cartel, kundi lililosumbua sana nchini Mexico.

Arturo Beltrán Leyva, alizaliwa September 27 mwaka 1961 huko katika mji wa Sinaloa nchini Mexico.

Kulikuwa na kesi nyingi dhidi ya kundi hilo, watu walikuwa wakiuawa, wanawake walibakwa, walisafirisha sana silaha kwenda sehemu mbalimbali, wengine waliteswa na kutekwa. Kwa kifupi, kundi hili lilikuwa hatari zaidi kuliko makundi mengine yaliyowahi kutokea huko nchini Mexico.

Arturo Beltrán Leyva aliuawa na wanajeshi wa majini mwaka 2009 katika majibizano ya kurushiana risasi na wanajeshi wa Mexico.

Felix Mitchell maarufu kama “The Cat”

Ni miongoni mwa wauza dawa zda kulevya wakubwa waliowahi kutokea duniani. Alikuwa na kundi lake liitwalo 69 Mob. Alianza kazi hiyo chini kwa chini na ilikuwa vigumu kukamatwa kwani alikuwa mjanja sana.

Alipokamatwa, alifungwa jela ila wakati akiwa ametumikia kifungo kwa miaka miwili, kuna jamaa hukohuko jela akamuua kwa kumchoma kisu, hiyo ilikuwa mwaka 1986 na mazishi yake yalihudhuriwa na watu wengi, sawa na mazishi ya aliyekuwa mwanaharakati, Martin Luther King Jr.

Amado Carrillo Fuentes maarufu kama “Lord of the Skies”

Alikuwa Mmexico aliyekuwa akifanya biashara ya dawa za kulevya kwa kiasi kikubwa. Hakuwa mkuu wa kitengo, aliajiriwa na bosi wake aliyeitwa Rafael Aguilar Guajardo akamgeukia kwa kumuua na kuchukua jukumu la kuongoza kitengo.

Ndiye muuzaji pekee wa dawa za kulevya aliyekuwa akiingiza kiasi kikubwa nchini Marekani kuliko mtu yeyote.

Alikuwa bilionea, mwenye kupenda watu na kusaidia masikini. Hakuwa na utani katika biashara hiyo, aliua wote aliohisi kwamba walikuwa watu wabaya katika biashara yake.

Alitumia ndege zake kusafirisha dawa za kulevya kwenda nchini Marekani mara nne kwa siku. Kumkamata haikuwa kazi nyepesi kwa sababu alikuwa akibadilisha sura yake kwa kuvaa sura ya bandia.

Mwaka 1997 alipokuwa akifanyiwa upasuaji wa kuwekewa sura bandia katika hospitali ya Santa Monica nchini Mexico, dawa zilizidi hivyo kufariki dunia na baada ya siku mbili, wale madaktari waliofanya upasuaji wa kumuwekea sura ya bandia wakakutwa wameuawa kinyama na miili yao kutupwa.

Pablo Escobar maarufu kama “The World’s Greatest Outlaw”

Ni Mcolombia aliyekuwa akiuza dawa za kulevya kwa kiasi kikubwa, alikuwa katili na hakusita kumfyeka yoyote aliyetishia kuingilia biashara zake. Hakutaka mchezo, hakuwahi kuweka fedha benki, alikuwa akizihifadhi ndani na wakati mwingine zilikuwa zikiliwa na panya.

Kuna kipindi mtoto wake alikuwa akiumwa, alizitumia dola za Kimarekani kumuwashia moto, eti kupoza baridi iliyokuwa ikimpiga, kitu kilichowakasirisha sana Wamarekani, waliona wamedharauliwa sana mpaka noti yao kuchomwa moto.

Alikuwa na utajiri mkubwa na mwaka 1989 alitangazwa kama tajiri wa saba duniani akiwa na utajiri wa dola bilioni 25, ambapo alikuwa akimiliki sehemu nne kati ya tano (4/5) ya soko kubwa la dawa ya kulevya duniani.

Pablo Escobar alikuwa akisafirisha tani 15 za dawa ya kulevya kila siku barani America, ambapo aliwaua majaji 30 waliokuwa wakisimamia kesi zake na polisi 400 ambao walionekana kimbelembele kumfuatilia kwenye biashara zake.

Aidha Pablo Escobar aliripua ndege aina ya Avianca Flight 203 ambayo ilikuwa ikimbeba waziri mkuu wa kipindi hicho nchini Colombia.

Kwa kifupi, jamaa alikuwa na pesa kiasi cha kuiambia serikali yake kwamba imuache afanye biashara zake na angelipa deni la dola bilioni 20 lililokuwa likidaiwa, ila serikali ikakaata na kumuua.

Joaquín Guzmán Loera maarufu kama “El Chapo Guzmán”

Joaquín Guzmán anaonekana kama mwamba wa biashara ya dawa za kulevya. Ni Mmexico mwenye mkwanja mrefu ambapo amekuwa akiupata kupitia biashara hiyo.

Alikuwa mtu anayetafutwa kwa nguvu zote kabla ya kukamatwa. Aliwekeza nguvu kubwa katika biashara hii, Wamarekani na Wamexico walimtafuta lakini hawakumpata.

Wakati wakiwa na uchungu naye, wakafanikiwa kumpata na hivyo kufungwa nchini Mexico. Kutokana na fedha alizokuwa nazo, inasemekana kwamba aliwahonga askari magereza na kutoroka kwa kupitia katika bomba la choo la chini kwa chini.

Wamarekani walikasirika sana, wakaahidi kumtafuta, kweli wakaingia kazini, hawakuchukua muda sana, wakamnasa na hivyo kuiambia Serikali ya Mexico kwamba watamfunga wao wenyewe ili wamuonyeshee kwamba wao si watu wa mchezo.

Kweli wakamfunga na mpaka leo hii yupo gerezani akiendelea kutumikia kifungo chake ambacho hakikuwekwa wazi ni cha muda gani.

MAONI YAKO