SERIKALI imetumia na inaendelea kutumia nguvu nyingi kwenye uwekezaji katika sekta ya utalii, ambapo matunda yake tunayaona, kwani utalii umekuwa sekta kiongozi katika uingizaji wa fedha za kigeni hapa Zanzibar.

Malengo yaliyopo ni kufikia watalii 500,000 ifikapo mwaka 2020, ambapo kutokana na kasi ya uingiaji wa watalii visiwani kwetu, tunaweza tukapindukia idadi hiyo kabla yakufikia mwaka huo.

Kwa hakika jitihada zinazochukuliwa katika kuutangaza utalii wetu nje ya nchi tunaziona, ambapo Kamisheni ya Utalii imekuwa ikishiriki maonesho mbalimbali ya utalii duniani.

Aidha suala la kutafuta masoko mapya ya utalii kama vile kutafuta watalii kutoka nchi za China, India, Urusi na sehemu nyengine kadhaa jitihada zimekuwa sikichukuliwa.

Pamoja na jitihada zote hizo, tungependa kueleza kwamba siri kubwa ya kuutangaza utalii ni kumtumia mtalii aliyeitembeleza nchi yetu kuwa balozi mzuri wa kuielezea nchi yetu baada ya kurudi kwao.

Kwa kawaida mtu yoyote anayefunga safari kwenye sehemu yoyote, baada ya kurudi nyumbani hupenda kueleza mazuri ambayo amekuyakuta na kufanyiwa na wenyeji wake.

Itakuwa jambo la kusikitisha sana na pale mtalii anaporudi nchini kwao kuwaeleza ndugu, jamaa na marafiki zake sifa mbaya tupu kuhusu Zanzibar badala ya mazuri mengi tuliyonayo.

Pengine mabaya hayo si miongoni katika utamaduni, silka zetu n ahata sifa zetu, lakini wale wachache wanaofanya hivyo humpa fursa mtalii kutujumuisha wananchi sote wa Zanzibar, kwa kueleza kuwa hizo ndizo sifa zetu.

Kwa mfano, kama mtalii ameamua kuitembelea Zanzibar kwa mapenzi makubwa aliyonayo, kwa bahati mbaya anavamiwa na vibaka anaporwa na hata kujeruhiwa, hivi tunafikiri akirudi kwao akahadithie zuri lipi?

Katika akili ya kawaida mtalii huyo akirudi kwao ataivisha nchi yetu sifa mbaya, kwa kuielezea nchi za majambazi, waporaji, vurugu na fujo, jambo ambalo halitawashawishi wengine wala kuwa na hamu kuja kutembelea nchini kwetu.

Aidha kama mtalii anatembelea kwenye fukwe zetu zenye mchanga safi mweupe ama amebarizi kwenye mchanga huo, lakini kwa bahati mbaya anajikuta anakanyaga ama kushika kinyesi, hivi akifika kwao akahadithie nini?

Bila shaka akifika kwao hadithi kubwa ni kwamba Zanzibar ni nchi ambayo watu wake hawatumii vyoo, hatosema kuwa baadhi ya wazanzibari, atajumuisha wananchi wote kuwa ni watu wasio na na vyoo.

Hili limekuwa tatizo kubwa kwenye sehemu za vijiji vilivyoko kando ya bahari ambapo watu wazima na nadhari zao, wakiwa na akili timamu wanaacha vyoo nyumbani na kwenda kujisaidia ufukweni.

Mfano mwengine kama mtalii ameshindwa kusoma ramani vizuri anatafuta mwenyeji amfahamishe anapokwenda, mwenyeji anayeulizwa hana mlahaka, hana tabasamu, hana muda wa kumsaidia, hivi atakwenda kutuhadithia vipi akifika kwao?

Lengo letu ni kubainisha changamoto hizi ili tujipange vizuri kwa sababu bila ya kuyashughilikia haya tunaweza kutumia nguvu kubwa kuutangaza utalii, lakini sifa zetu mbaya ndio zinawafanya watalii wasiingie nchini.

Kitu cha muhimu cha kukumbushana ni lazima tuhakikishe watalii wetu wanaoingia nchini tuwafanye kuwa mabalozi wa kuitangaza vyema nchi yetu hapo ndipo tutakapo yashuhudia mafuriko ya wataalii.

MAONI YAKO